• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 1:51 PM
Bayern wana kiu ya kutwaa Kombe la Dunia kwa Klabu nchini Qatar ili kuweka historia – Lewandowski

Bayern wana kiu ya kutwaa Kombe la Dunia kwa Klabu nchini Qatar ili kuweka historia – Lewandowski

Na MASHIRIKA

ROBERT Lewandowski anaamini kwamba Bayern Munich wana uwezo wa kupepeta Tigres UANL ya Mexico kwenye fainali ya Kombe la Dunia kwa Klabu mnamo Februari 11, 2021, nchini Qatar na kuweka historia katika ulingo wa soka.

Wafalme hao wa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) watakuwa wa pili baada ya Barcelona kutia kapuni mataji yote sita katika mashindano ya soka ya nyumbani na mechi za kimataifa iwapo watawazidi ujanja Tigres.

Kufikia sasa, Bayern tayari wametia kibindoni ubingwa UEFA, Super Cup, German Super Cup, Bundesliga na German Cup.

Tigres waliweka historia ya kuwa klabu ya kwanza kutoka Mexico kuwahi kufuzu kwa fainali ya Kombe la Dunia baada ya kuchabanga Palmeiras ya Brazil 1-0 kwenye nusu-fainali. Klabu hiyo ndiyo ya kwanza kutoka Shirikisho la Soka la Amerika Kaskazini, Amerika ya Kati na Caribbean (Concacaf) kuwahi kutinga fainali ya Kombe la Dunia.

“Kombe la Dunia ni nyongeza nzuri kwa mengi ambayo tayari tumejinyakulia,” akasema Lewandowski ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Poland.

Fainali za Kombe la Dunia kwa Klabu nchini Qatar zinatumiwa kufanyia majaribio ya fainali za Kombe la Dunia kwa mataifa zitakazoandaliwa nchini Qatar mnamo 2022.

“Fainali ijayo kwetu ina maana kwamba tunaweza kutia kapuni taji letu la sita. Ushindi utakuwa na historia kubwa katika ulingo wa soka,” akaongeza Lewandowski.

“Tuko tayari kuandikisha historia ingawa kibarua kilichopo mbele yetu si chepesi. Tutajituma. Ukiwa karibu namna hiyo kunusia ubingwa, basi itabidi tu utie bidii na kuunyanyua,” akaongeza fowadi huyo.

Pigo la pekee kwa Bayern ni kutokuwepo kwa viungo Leon Goretkza na Javi Martinez waliopatikana na virusi vya corona kabla ya kikosi chao kinachonolewa na kocha Hansi Flick kufunga safari ya kuelekea Qatar.

Mabao mawili yaliyofungwa na Lewandowski kwenye nusu-fainali dhidi ya Al Ahly ya Misri mnamo Februari 8, 2021 yalisaidia Bayern kuwa pua na mdomo kujinyanyulia taji la sita la haiba kubwa chini ya kipindi cha miezi tisa.

Lewandowski kwa sasa anajivunia mabao 29 kutokana na mechi 27 ambazo amechezea Bayern hadi kufikia sasa msimu huu.

“Tulikuja nchini Qatar kutwaa Kombe la Dunia. Kwa kuwa kwa sasa tumekaribia kufikia ufanisi huo, tuna kila sababu ya kujitahidi ili kuweka hai matumaini yetu,” akasema fowadi wa Tigres, Carlos Gonzalez.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

You can share this post!

AFROBASKET: Kenya Morans yalenga kumaliza ukame wa miaka 28

Pwani ina wanariadha wa mbio, kinachohitajika ni mikakati...