• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
Maandamano yazuka nchini Sudan kuhusu uchumi, bei za bidhaa

Maandamano yazuka nchini Sudan kuhusu uchumi, bei za bidhaa

Na AFP

KHARTOUM, Sudan

MAANDAMANO yalizuka katika sehemu kadhaa nchini Sudan kutokana na hali ngumu ya uchumi na kupanda kwa gharama ya maisha.

Hii ni licha ya Amerika kueleza kuunga mkono juhudi za serikali mpya ya taifa hilo kufufua uchumi wake.

Mnamo Jumanne, waandamanaji walikabiliana vikali na polisi katika mji wa Nyala, ulio makao makuu ya jimbo la Darfur Kusini.

Waandamanaji hao waliwarushia polisi mawe na kuchoma maduka kadhaa yaliyo kwenye soko kuu mjini humo.

“Tumekataa bei za juu, tumekataa njaa!” wakasema.

Kutokana na maandamano hayo, idara za usalama zimeweka kafyu kutoka saa 12 jioni hadi saa 12 asubuhi.

Maandamano mengine yalitokea katika mji wa Port Sudan, ulio karibu na Ziwa Shamu, hali ilyolazimu shule kadhaa na maduka kufungwa.

Maandamano pia yalitokea katika majimbo ya Kordofan Kaskazini na Al-Obeid, kulingana na shirika la habari la serikali nchini humo, SUNA.

Katika siku za hivi karibuni, maandamano makubwa pia yamekuwa yakishuhudiwa katika jiji kuu, Khartoum na jimbo la Gedaref, lililo mashariki mwa jiji hilo.

Baraza jipya la mawaziri linajumuisha watu waliohudumu kama viongozi wa waasi, ambapo jukumu lake kuu litakuwa ufufuzi wa uchumi.

Uchumi wa taifa hilo unaelezwa kudorora kutokana na vikwazo ilivyokuwa imewekewa na Amerika kwa muda mrefu, usimamizi mbaya na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka wakati wa utawala wa rais wa zamani, Omar el Bashir. Bashir aling’olewa mamlakani mnamo 2019.

Sudan imekuwa ikipitia misukosuko ya kisiasa tangu Aprili 2019, wakati Bashir aling’olewa mamlakani.

Kiongozi huyo aling’atuka kutokana na maandamano makubwa dhidi ya utawala wake kwa kushindwa kufufua uchumi na kudhibiti ongezeko la bei za mkate.

Jumatatu, Waziri Mkuu Abdalla Hamdok alitangaza baraza jipya la mawaziri, linalomjumuisha mwanauchumi Gibril Ibrahim kama Waziri wa Fedha. Ibrahim alikuwa kiongozi wa waasi kabla ya uteuzi huo.

“Tunawaahidi kufanya kila tuwezalo kuhakikisha tumepunguza bei za mikate na mafuta. Mbali na hayo, tutaimarisha huduma za afya kwa kuhakikisha kila mmoja anafikiwa nazo,” akasema waziri huyo kwenye mtandao wa Twitter baada ya uteuzi wake.

Hapo Jumanne, Hamdok alizungumza kwa njia ya simu na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Amerika, Antony Blinken, aliyeeleza kuunga mkono serikali hiyo ya mpito.

Kupitia ujumbe alioweka kwenye Twitter, Hamdok alisema Amerika imejitolea kuunga mkono juhudi za kutafuta amani na demokrasia nchini humo.

“Amerika pia itatusaidia kuimarisha ushirikiano wetu kiuchumi,” akasema.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Amerika ilisema wawili hao “walijadili kuhusu njia za kuendeleza mageuzi ya kiuchumi na maendeleo na utekelezaji wa mikataba ya amani iliyofikiwa majuzi. Waliangazia pia kiini cha mapigano eneo la Darfur na juhudi za kuyamaliza.”

You can share this post!

Wembe ‘ule ule’ ndio uliomnyoa Kang’ata

TAHARIRI: Suluhu si kufunga shule za mabweni