• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
TAHARIRI: Suluhu si kufunga shule za mabweni

TAHARIRI: Suluhu si kufunga shule za mabweni

KITENGO CHA UHARIRI

PENDEKEZO la kufunga shule za bweni nchini linahitaji kufanyiwa darubini ya kina zaidi na wadau wakuu wa sekta ya elimu ili kuzuia madhara.

Gharama ya miundomsingi ya shule hizi ni ya juu mno hivi kwamba wazo la kuzifunga linafaa kujadiliwa kwa uangalifu mkubwa. Si ujenzi tu, bali pia ununuzi wa vifaa vya shule za mabweni umegharimu serikali, wazazi na mashirika mbalimbali ya ufadhili kima kikubwa cha pesa.

Si siri kwamba shule za kitaifa zimejengwa kwa pesa za mlipaushuru. Shule kubwa na nzuri kama hizo kubadilishwa ili kuwa shule za kutwa kunamaanisha kuwa, wanafunzi watalazimika kujitafutia makazi karibu na shule; jambo ambalo ni changamoto sugu inayoweza kuleta maafa makubwa. Bila shaka wanafunzi hao watalazimika kuishi na jamii inayoizingira shule yao.

Hatari kuu zaidi ni kuwa wanafunzi wenye utovu wa nidhamu wanaweza kuvurugika zaidi kimaadili ama kuathiri jamii kwa njia hasi. Chukulia mfano wa mwanafunzi mwenye tatizo la ukosefu wa nidhamu, kisha aanze kuishi peke yake katika chumba alichokodishiwa na wazazi karibu na shule. Maadili ya mwanafunzi huyo yataharibika na huenda asimalize shule itakiwavyo.

Isitoshe, shule kama hizi husajili wanafunzi wanaoishi maeneo wanamotoka. Halitakuwa jambo zuri kutosajili wanafunzi kutoka maeneo mengine kwa sababu ya ukosefu wa mabweni. Taasisi ya Kuunda Mitaala nchini (KICD) inapaswa kubuni somo ambalo litawafundisha wanafunzi jinsi ya kuishi na wanajamii wengine.

Wanafunzi wanahitaji kuheshimu wakubwa wao na watu wengine wenye mamlaka juu yao. Wanafunzi pia wafundishwe kujiheshimu na kuheshimiana wao kwa wao.

Kuwaondoa wanafunzi katika shule za mabweni na kutoshughulikia kiini cha visa vya moto shuleni, ni kuahirisha matatizo ambayo yatarudi kututafuna sisi wenyewe na wadau wa sekta ya elimu kwa jumla.

Shule nyingi zimekuwa zikichomwa katika siku za hivi karibuni na matukio haya yanahitaji kudhibitiwa, la sivyo balaa kuu zaidi itatuambata.

Suluhu la kudhibiti corona na utovu wa nidhamu shuleni si kufunga shule za bweni. Shule zifuate maagizo ya Wizara ya Afya kuhusu jinsi ya kudhibiti corona. Usafi udumishwe, kamera za CCTV ziwekwe, vifaa viboreshwe, na kudhibiti matumizi ya mihadarati shuleni.

Wakuu wa shule wanapaswa kufanya kazi pamoja na wazazi na serikali ili kulinda mustakabali wa watoto wao.

You can share this post!

Maandamano yazuka nchini Sudan kuhusu uchumi, bei za bidhaa

KAMAU: Manamba: Huu uhuni sasa umepita mipaka