KAMAU: Manamba: Huu uhuni sasa umepita mipaka

Na WANDERI KAMAU

NIKIWA katika shule ya msingi karibu miaka 20 iliyopita, babangu alifanikiwa kununua matatu.

Binafsi, nilijiambia hiyo ilikuwa hatua muhimu sana katika maisha yake kwani lilikuwa jambo kubwa kumiliki gari enzi hizo.

Aliyemiliki gari alionekana na kuheshimika kama ‘tajiri’ kotekote vijijini. Alialikwa katika karibu kila hafla “kutoa mashauri” kwa vijana kuhusu mielekeo wanayopaswa kufuata ili kufanikiwa maishani.

Ingawa baba baadaye aliliuza gari hilo na kuegemea biashara zingine, hilo halikuondoa wala kushusha hekima yake.

Si baba tu. Wale waliomiliki magari kijijini mwetu waliheshimika sana. Gari lilikuwa kama ishara ya maarifa na ufanisi mkubwa.

Ni wazi kuwa hadi sasa, wanaomiliki magari bado wanaheshimika licha ya nyakati kubadilika sana.

Kimsingi, kuna hekima fulani inayotokana na umiliki ama uendeshaji magari, hasa yanayowabeba abiria.

Kinaya ni kwamba, hekima hiyo inaendelea kushuka tofauti na ilivyokuwa zamani.

Sekta ya matatu imegeuka kuwa uwanja wa fujo, ujambazi, ukatili, mateso na dhuluma za kila aina.

Kinyume na awali ambapo uhusiano wa wahudumu na abiria ulikitwa kwenye hekima, uungwana na upole; hali sasa imegeuka kuwa kama ushindani wa maadui wawili.

Manamba huwaona abiria kama vinyago tu, wanaopaswa kufuata kila maagizo wanayowapa.

Wao hujiona kama ‘wafalme’ au ‘miungu’ wadogo wanaofaa kutoa usemi wa mwisho kuhusu vile sekta inapaswa kusimamiwa na kuendeshwa.

Huwa wamejaa matusi na dharau. Wengine ni wajeuri bila sababu zozote maalum.

Baadhi hata wamekuwa kaidi kiasi cha kutowaogopa polisi kwani wanajua namna ya “kuwakabili.”

Bila shaka, ukosefu wa mikakati ya kudhibiti sekta hii muhimu imechangia pakubwa kuifanya kuwa kama Sodoma na Gomorra.

Ni sekta iliyojaa ghasia, mafarakano na ushindani – ambao chanzo chake hakijulikani.

Sekta hiyo inahusishwa na ukatili wa kina aina. Si ulanguzi wa mihadarati, wizi wa mabavu, ubakaji, utekajinyara. Hata baadhi ya matatu zinadaiwa kudhibitiwa na magenge ya wahalifu!

Ni sekta imepoteza hadhi yake, kinyume na ilivyokuwa enzi ya Mzee Jomo Kenyatta ambapo serikali yake iliyaagiza mabenki kuwapa wawekezaji mikopo ili kuikuza.

Mzee Kenyatta alitoa agizo hilo ili kuwapa Wakenya wa kawaida nafasi ya kuwekeza katika sekta ya uchukuzi.

Kabla ya hapo, ni mabasi makubwa pekee yaliyohudumu kwenye uchukuzi wa abiria, na yalihusishwa na watu matajiri pekee.

Tangu miaka ya sabini sekta ya matatu imekua kwa kasi kubwa sana, ambapo sasa ni miongoni mwa zile zinazotoa ajira kwa idadi kubwa ya Wakenya, hasa vijana.

Cha kusikitisha ni hatua ya serikali kunyamazia vitendo vya kutamausha vinavyofanywa na wahudumu kwa abiria panapoibuka mzozo kuhusu nauli.

Wengi wamefia mikononi mwa wahudumu katili baada ya kurushwa nje ya matatu, sababu tu ya tofauti ndogo kama nauli.

Mamia ya wanawake nao wamelalamika kubakwa au kudhulumiwa kimapenzi na manamba walaghai wasio utu. Manamba wamegeuka ‘miungu’ wasiogusika Je, nani ataukabili uhuni huu?

akamau@ke.nationmedia.com

 

Habari zinazohusiana na hii