KING’ORI: Heshima imewatoka waheshimiwa, hawaoni aibu!

Na KINYUA KING’ORI

SARAKASI ambazo tumeanza kushuhudia ambapo wanasiasa wanatumia hafla za mazishi kuzua fujo zinafaa kukomeshwa haraka, la sivyo kampeni za 2022 zitakuwa mbovu sana.

Juma lililopita katika mazishi ya babake Joash Mangi, ambaye ni Naibu Gavana wa Kisii, wabunge Silvanus Osoro (Mugirango Kusini) na Simba Arati (Dagoretti Kaskazini) walikabiliana hadharani na kurushiana ngumi mbele ya waombolezaji wakiwemo Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Kitendo hicho kilichotokea kijijini Tendere, eneobunge la Bomachoge Chache, kinafaa kiwe chanzo cha serikali kuingilia kati kuzima siasa mazishini hasa wakati huu wa kuvumisha Mswada wa BBI na kuanza kwa kampeni za 2022.

Alipohutubia waombolezaji, Arati alimghadhabisha Osoro kwa kauli yake iliyomlenga kinara wa “mahasla”; akimtaka Ruto kuomba jamii ya Kisii msamaha kutokana na machafuko yaliyokumba taifa baada ya uchaguzi mkuu 2007. Kulingana na Arati, watu wa jamii yake waliangamia katika bonde la Ufa.

Matamshi hayo yalimchemsha Osoro kiasi cha kupanda jukwaani kumzima Arati; ambapo walianza kutusiana na kurushiana makonde bila kuona aibu.

Tabia ya wanasiasa kugeuza mazishi kuwa majukwaa ya kuchapa siasa imekithiri katika maeneo yote nchini, hasa mashambani ambako visa vingine hata havitangazwi na vyombo vya habari.

Mwezi jana kisa sawia kilitokea eneobunge la Igembe Kaskazini wakati wafuasi wa mbunge wa hapo, Maoka Maore, mtangulizi wake Joseph M’eruaki na aliyekuwa katibu wa Chama cha Walimu (KNUT) tawi la Nyambene, Julius Taitumu, walizua fujo kwa kutumia makundi ya vijana kuvuruga mazishi na kuendesha siasa zao duni.

Wanasiasa wanafaa kunyimwa fursa kuhutubia waombolezaji ikiwa wataendelea na tabia hii potovu kwani wameshindwa kujidhibiti.

Je, ikiwa viongozi wanaweza kwenda kinyume na maadili mema mbele ya umma tena mchana wa jua, watarajia watoto wa Kenya wawe wenye nidhamu?

Viongozi wakitaka kupiga siasa waandae mikutano yao mahususi badala ya kutegemea hafla za mazishi.

Hata wanaotamani kuwa wagombeaji katika uchaguzi wa 2022 waweke kipaumbele kuuza sera zao kwa wananchi, kueleza jinsi watabadilisha makosa ya viongozi waliopo iwapo watachaguliwa, badala ya kutumia vijana kuzua fujo na matusi.

Kinachotia hofu zaidi ni kwamba kadri uchaguzi unapokaribia ndivyo wanasiasa wanazidi kupandisha joto la kisiasa nchini kuanzia mijini hadi vijijini.

Iwapo serikali itashindwa kuvalia njuga swala hili mapema, kwa kuwachukulia hatua kali viongozi wachochezi na wakosa adabu, huenda uchaguzi wa 2022 ukakumbukwa na machafuko kama ya 2007.

Ni wajibu wa serikali kutumia kila mbinu kudumisha usalama nchini, na wanasiasa wanaotumia vijana au wafuasi wao kuzua fujo wakamatwe na kushtakiwa.

Nakubaliana na Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) kwamba viongozi wachochezi wazimwe kuwania nyadhifa za umma.

Tume ya NCIC ili kufaulu, inafaa kushirikiana na vyama vya kisiasa na Tume huru ya Uchaguzi na mipaka (IEBC) kuwazuia kuwania nyadhifa zozote za kisiasa.

Wananchi tunaamini sasa,wanasiasa wachochezi hawataruhusiwa katika chaguzi zijazo ikiwemo 2022. Hii itawapiga breki wanasiasa wanafiki wanaopenda kutumia fujo na ghasia kuchaguliwa kuwa viongozi.

Wabunge Arati na Osoro walipaswa kuwa tayari wameshtakiwa kwa kupigana hadharani.

Serikali ibuni mikakati kabambe kutoa suluhu juu ya tabia hiyo, nakubaliana na Tume ya uwiano na utangamano ya kitaifa (NCIC) inayoongozwa na Bw, Samuel Kobia kwamba viongozi wachochezi watazimwa kuwania nyadhifa za umma.

Tume ya NCIC ili kufaulu, inafaa kushirikiana na vyama vya kisiasa na Tume huru ya Uchaguzi na mipaka (IEBC) kuwazuia kuwania nyadhifa zozote za kisiasa.

Wananchi tunaamini sasa,wanasiasa wachochezi hawataruhusiwa katika chaguzi zijazo ikiwemo 2022. Hii itawapiga breki wanasiasa wanafiki wanaopenda kutumia fujo na ghasia kuchaguliwa kuwa viongozi.

Habari zinazohusiana na hii