• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Atalanta yadengua Napoli na kujikatia tiketi ya kuvaana na Juventus kwenye fainali ya Coppa Italia msimu huu

Atalanta yadengua Napoli na kujikatia tiketi ya kuvaana na Juventus kwenye fainali ya Coppa Italia msimu huu

Na MASHIRIKA

ATALANTA kwa sasa watavaana na Juventus kwenye fainali ya Coppa Italia msimu huu baada ya kuwapepeta Napoli 3-1 kwenye mkondo wa pili wa nusu-fainali ya kipute hicho Februari 10, 2021.

Vikosi hivyo vilishuka dimbani kwa mchuano wa marudiano baada ya kuambulia sare tasa kwenye mechi ya mkondo wa kwanza iliyowakutanisha jijini Naples wiki moja iliyopita.

Mnamo Jumatano usiku, Duvan Zapata aliwaweka Atalanta kifua mbele katika dakika ya 10 kupitia kombora alilovurumisha kutoka hatua ya 25 kabla ya kuhusika moja kwa moja kwenye magoli mengine mawili yaliyofumwa wavuni na Matteo Pessina.

Zapata alimwandalia Pessina krosi safi katika dakika ya 16 kabla ya Hirving Lozano kuwafungia Napoli bao la kufutia machozi kunako dakika ya 53. Goli la tatu la Atalanta lilipachikwa wavuni na Pessina dakika 12 kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa.

Atalanta ambao walizidiwa maarifa na Lazio kwenye fainali ya Coppa Italia mnamo 2019, wametia kibindoni kombe moja pekee la haiba katika historia yao ya kushiriki soka. Taji hilo lilikuwa la Coppa Italia mnamo 1963.

Licha ya historia hiyo, Atalanta wamekuwa miongoni mwa vikosi vya kuogopewa sana na wapinzani wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) na bara Ulaya (UEFA) katika kipindi cha misimu miwili iliyopita. Hii ni baada ya kikosi hicho kutinga robo-fainali za UEFA mnamo 2020.

Juventus waliopigwa na Napoli kwenye fainali ya Coppa Italia mnamo 2020, walifuzu kwa fainali ya msimu huu mnamo Februari 9, 2021 baada ya kuwabandua Inter Milan kwa mabao 2-1. Fainali ya muhula huu wa 2020-21 imeratibiwa kusakatwa Mei 19.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Sevilla wapepeta Barcelona kwenye mkondo wa kwanza wa...

Iheanacho atokea benchi na kuokoa chombo cha Leicester City...