• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 10:55 AM
Mvua ya mabao Everton wakidengua Tottenham kwenye raundi ya tano ya Kombe la FA kwa magoli 5-4

Mvua ya mabao Everton wakidengua Tottenham kwenye raundi ya tano ya Kombe la FA kwa magoli 5-4

Na MASHIRIKA

EVERTON walitinga hatua ya nane-bora kwenye kampeni za Kombe la FA msimu huu baada ya kuwapokeza Tottenham Hotspur kichapo cha 5-4 mnamo Februari 10, 2021 uwanjani Goodison Park.

Mchuano huo ulikuwa wazi kwa kikosi chochote kushinda kabla ya vijana wa kocha Carlo Ancelotti kujituma maradufu katika muda wa ziada na kupata bao la ushindi kupitia kwa Bernard Duarte, 28.

Spurs walitamalaki mchezo katika dakika za mwanzo wa kipindi cha kwanza na juhudi zao zikazaa matunda kupitia kwa Davinson Sanchez aliyewaweka kifua mbele katika dakika ya tatu.

Hata hivyo, Dominic Calvert-Lewin aliyeondolewa baadaye uwanjani kutokana na jeraha la paja, aliwasawazishia Everton katika dakika ya 36 kabla ya Richarlson Andrade kufanya mambo kuwa 2-1 baada ya kumzidi ujanja kipa Hugo Lloris kunako dakika ya 38.

Ingawa Gylfi Sigurdsson alifungia Everton penalti katika dakika ya 43, Erik Lamela aliwarejesha Spurs mchezoni sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa kipindi cha kwanza kupulizwa.

Sanchez alifungia Spurs bao la tatu katika dakika ya 57 kabla ya Richarlson kuwarejesha Everton uongozini dakika 11 baadaye.

Kocha Jose Mourinho alimleta uwanjani fowadi na nahodha Harry Kane aliyefungia Spurs bao la nne na la kusawazisha mwishoni mwa kipindi cha pili na kumweka refa katika ulazima wa kuamua mshindi wa mechi hiyo katika muda wa ziada.

Ingawa ushirikiano mkubwa kati ya Kane na Son Heung-min ulikuwa tishio kubwa kwa Everton, masogora wa Ancelotti walisalia imara na wakaanza kuvamia lango la wageni wao kwa kushtukiza.

Ilikuwa hadi dakika ya 97 ambapo Bernard aliwafungia Everton bao la ushindi baada ya kukamilisha krosi ya Sigurdsson kwa ustadi mkubwa.

Everton wanafukuzia taji lao la kwanza katika soka ya Uingereza tangu 1995 walipotawazwa mabingwa wa Kombe la FA. Wakati huo, waliwadengua Spurs kwenye hatua ya nusu-fainali na kutwaa ubingwa wa taji hilo.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa kikosi kinachonolewa na Mourinho kufungwa mabao matano katika mechi moja tangu waliokuwa waajiri wake Chelsea wapigwe 5-3 na Spurs kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Januari 2015. Wakati huo, Spurs walikuwa chini ya kocha Mauricio Pochettino ambaye kwa sasa anadhibiti mikoba ya Paris Saint-Germain (PSG) nchini Ufaransa.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Nakuru yashinda Siaya michuano ya majaribio ya...

Okutoyi afika Casablanca salama kukuza talanta yake ya...