• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
Muthama, Kalonzo wakashifiwa kwa kujibizana haflani

Muthama, Kalonzo wakashifiwa kwa kujibizana haflani

Na KITAVI MUTUA

VIONGOZI kadhaa wa kisiasa na kidini katika eneo la Ukambani, Alhamisi walikashifu vikali majibizano ya kisiasa kati ya kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka na aliyekuwa Seneta wa Machakos, Johnson Muthama mnamo Jumatano.

Askofu Abraham Mulwa wa kanisa la African Inland Church (AIC) alisema ilikuwa taswira ya kusikitisha kuwaona viongozi hao wakijibizana kuhusu masuala yanayohusu familia, ambapo nusura wapigane hadharani.

“Lilikuwa jambo la kusikitisha. Kinachoshangaza zaidi, Mabwana Musyoka na Muthama ni washirika wa kanisa la AIC, na wanajua msimamo wa kanisa kuhusu uendeshaji wa siasa katika mazishi na hafla zingine za kanisa,” akasema Askofu Mulwa, Alhamisi kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Askofu alisema ametuma kundi la wazee kwa viongozi hao wawili ili kuwazungumzia na kuwakumbusha kuhusu athari za kuonyesha mifano kama hiyo kwa viongozi wachanga.

Hapo Jumatano, kizaazaa kilizuka katika eneo la Mitamboni, Kaunti ya Machakos, ambapo nusura Bw Muthama ampige Bw Musyoka wakati wa mazishi ya Askofu Bernard Nguyu. Marehemu ndiye alikuwa msimamizi mkuu wa kanisa katika eneo hilo.

Kwenye kisa hicho kilichowashangaza waombolezaji, Bw Muthama aliondoka kwenye kiti chake kwa ghadhabu, lakini akazuiwa kufika alikokuwa Bw Musyoka, ambaye alikuwa akihutubu.

Bw Musyoka alimkejeli Bw Muthama kwa msururu wa semi zilizoangazia ndoa iliyovunjika kati yake na mkewe wa zamani, Bi Agnes Kavindu.

Bw Musyoka alisema atamrejesha Bi Kavindu kwa Bw Muthama baada ya (Bi Kavindu) kuchaguliwa kama Seneta wa Machakos kwenye uchaguzi mdogo uliopangiwa kufanyika Machi 18.

Bi Kavindu anawania kiti cha useneta Machakos kwa tiketi ya Wiper.

Askofu huyo, ambaye alikuwa akiongoza hafla hiyo, alisema ni Kenya pekee ambako siasa huwa zinatawala mazishi, badala ya kuwa wakati wa kuifariji familia iliyofiwa.

Wengine waliokashifu tukio hilo ni mwenyekiti wa chama cha Maendeleo ya Wanawake katika kaunti hiyo Bi Francisca Mutinda, Gavana Kivutha Kibwana (Makueni) na mbunge Charles Kilonzo (Yatta).

Bi Mutinda alimkosoa vikali Bw Musyoka kwa kumchokoza Bw Muthama bila sababu yoyote ili kumwaibisha hadharani.

“Majizibazo hayo yameibua masuala mazito sana kuhusu maadili. Ni wazi kuwa Bw Musyoka analenga kutumia talaka kati ya Bw Muthama na Bi Kavindu kama njia ya kulipiza kisasi tofauti za kisiasa baina yake na Bw Muthama,” akasema Bi Mutinda.

Vile vile, alishangaa kuhusu sababu ambapo Bi Kavindu anakubali kutumiwa na viongozi wengine kisiasa ili kumkejeli Bw Muthama.

“Kumwambia mwanamume hadharani kwamba utamrejeshea mkewe baada ya muda fulani ni matusi mazito sana kulingana na tamaduni za Kiafrika. Hivyo, tunamtaka Bw Musyoka kuwaomba msamaha wenyeji wa Machakos kwa kumkejeli Bw Muthama,” akasema.

Prof Kibwana na Bw Kilonzo waliyakashifu vikali matamshi ya Bw Musyoka wakiyataja kukiuka mipaka ya kifamilia.

Uchaguzi huo unaonekana kuwa ushindani kati ya Bi Muthama, waziri wa zamani Mutua Katuku, anayewania kwa tiketi ya Maendeleo Chap Chap na Bw Urbanus Ngengele wa UDA, anayeungwa mkono na Bw Muthama.

You can share this post!

Joho, Kingi mbioni kufufua jumuiya ya Pwani

Nyachae asifiwa kwa ushujaa wake kisiasa