• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:45 AM
Amerika yatoa tahadhari kuhusu corona Tanzania

Amerika yatoa tahadhari kuhusu corona Tanzania

Na AFP

DAR ES SALAAM, Tanzania

SERIKALI ya Amerika imeonya kwamba maambukizi ya virusi vya corona yanaendelea kuongezeka kwa kiwango cha kutisha katika taifa jirani la Tanzania.

Ubalozi wa Amerika nchini humo umetoa kauli hiyo wiki moja tu baada ya nchi hiyo yenye uchumi mkubwa zaidi duniani kutoa tahadhari kwa raia wake dhidi ya kusafiri hadi Tanzania.

“Ubalozi wa Amerika unafahamu kuhusu kupanda kwa kiasi kikubwa kwa virusi vya corona nchini Tanzania. Hii ni licha ya serikali kuacha kutoa takwimu miezi michache baada ya corona kuchipuka mwaka 2020,” ikasema taarifa kutoka ubalozi huo.

Kwenye tahadhari hiyo, ubalozi huo ulisema kwamba kanuni au masharti ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona, hayazingatiwi tena nchini Tanzania.

Mara ya mwisho ambapo serikali ya Rais John Pombe Magufuli ilitoa takwimu ya mwisho kuhusu maambukizi ya corona na vifo vilivyotokana na ugonjwa huo ni mnamo Aprili mwaka jana.

“Hospitali na vituo vingine vya kiafya huenda vikalemewa kukidhi idadi kubwa ya wagonjwa wanaofika huko kupata matibabu ya corona. Pia vifo vinaendelea kuongezeka na hali huenda ikawa mbaya zaidi iwapo serikali haitachukua hatua zozote kutokomeza virusi hivyo,” ukaongeza ubalozi huo.

Hata hivyo, haukufichua au kutoa takwimu za maambukizi hayo, ikisisitiza tu kwamba janga hilo sasa limekithiri sana Tanzania.

Kituo Kikuu cha Kupambana na Magonjwa nchini Amerika nacho kiliwashauri raia wake wasije Tanzania na kuwataka walioko huko kuchukua tahadhari kutokana na uwepo wa corona.

Wiki jana, Wizara ya Afya ilikanusha kwamba maambukizi ya corona yamepanda na kuwa hospitali za nchi hiyo zimelemewa. Badala yake ilisisitiza kuwa hospital hizo zimekuwa zikiwahudumia wagonjwa wa maradhi mbalimbali wala si corona pekee.

Hata hivyo, Rais Magufuli amekuwa akiwataka raia waendelea na shughuli zao kama kawaida akisema kuwa nchi hiyo ilivishinda vita dhidi ya corona kupitia maombi na uwezo wake mwenyezi mungu.

Aidha wakati ambapo serikali za mataifa mengine ziliweka kafyu ya kutotoka nje, maisha ya raia wa Tanzania yalikuwa yakiendelea kama kawaida huku Rais wao akisema lengo lake ni kuimarisha uchumi wa nchi hiyo.

Pia Rais Magufuli mwaka jana alitilia shaka vipimo vilivyokuwa vikitumika akidai vilikuwa na kasoro na pia vilikuwa vitoa matokeo ya uongo.

You can share this post!

Majaji waogopa kazi ya Maraga

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Shirk ni dhambi lililo juu kabisa ya...