TAHARIRI: Serikali itoe ushauri nasaha kwa umma

KITENGO CHA UHARIRI

VISA vya watu kujichukulia sheria mikononi vimeongezeka tangu mwaka huu uanze.

Mtindo unaosuhudiwa ni kuwa, hata watoto wadogo wamekuwa wakiua wenzao au kujiua kutokana na mambo ambayo yanaweza kusuluhishwa.

Kisa cha punde zaidi ni cha mwanamke aliyeamua kuichoma nyumba, eti kwa sababu mumewe aliamua kuoa mke wa pili. Inasemekana kuwa mama huyo alikerwa na mpango wa mumewe kutaka kuchukua mke mwengine. Walizozana na huyo mama akaenda kukaa kwa rafikiye, kabla ya kurejea nyumbani na kuichoma.

Katika Kaunti ya Nakuru, mwanaume alimuua mkewe walipozozana na kijana wake kuhusu uuzaji wa mahindi ya kilo kumi. M wanaume huyo alitaka kuuza mahindi hayo lakini mkewe na mwanawe wa miaka 18 walipinga wazo hilo. Inasemekana jamaa huyo alikasirika na kumfyatulia kijana wake mshale. Kwa bahati mbaya, mshale huo ulimkosa kijana na kumfuma mkewe.

Visa hivi ni sehemu tu ya msururu wa matukio ambapo watu wamekuwa na hasira za kupita kiasi.

Jambi hili ni hatari kwa nchi, hasa ikizingatiwa kuwa tunaelekea kwenye msimu wa watu kuchochewa na siasa. Imebaki miezi 18 kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka ujao. Kabla ya hapo, kutakuwa na kampeni za kuamua kuhusu Mswada wa BBI, unaolenga kufanyia marekebisho Katiba. Tayari jana katika Bunge la Kaunti ya Baringo, madiwani walizua vurumai kuhusiana na mswada huo.

Ingawa Tume ya Uwiano na Utangamano (NCIC) imejitokeza na sera mbalimbali za kukabili ghasia na kutovumiliana kisiasa, huenda tatizo hili likaendelea kwa muda.

Inavyoonekana, matukio ya mwaka mmoja uliopita ambapo janga la corona liliathiri uchumi na maisha ya mamilioni ya watu, huenda yamechangia msongo wa mawazo.

Hasira zinazoonekana miongoni mwa watu wa tabaka mbalimbali, huenda ikawa si za kawaida.

Mbali na wizara ya Afya kuwahimiza Wakenya kuzingatia kanuni za kudhibiti msambao wa corona, inapaswa kuanzisha mpango wa kuwapa ushauri nasaha wananchi.

Maafisa wa Saikolojia wanapaswa kushirikishwa katika mpango huo wa kuzitembelea familia na kujadili kuhusu njia bora za kudhibiti athari za msongo wa mawazo. Jukumu la maafisa hao katika kuponya makovu yaliyosababishwa na ugonjwa huu wa kimataifa, ni kubwa na linalofaa kutekelezwa kama suala la dharura.

Habari zinazohusiana na hii