MATHEKA: Serikali inafanya vyema kuwafaa wanafunzi wajawazito

Na BENSON MATHEKA

HATUA ya serikali kuhakikisha kwamba wanafunzi wasichana wanaopata mimba wanaruhusiwa kuendelea na masomo, inafaa kuungwa mkono licha ya changamoto zinazowakabili kwa kuwa wazazi wachanga.

Hii itasaidia wasichana hao kupata nafasi ya kuwa na maisha bora siku zijazo, kama wenzao wavulana.

Kuna sababu nyingi zinazowafanya wanafunzi hao wa kike kupata mimba; mojawapo ikiwa ni umasikini.

Kama jamii hatufai kutoa kauli zinazoweza kuwakosesha matumaini maishani. Kuwalaumu hakutawasaidia kamwe.

Mchango wa wasichana waliopata elimu katika jamii hauwezi kupuuzwa kamwe.

Kuna waliopata mimba wakiwa wadogo lakini kwa sababu familia zao na jamii ziliwasaidia na kuwashika mkono, wamebobea katika sekta mbalimbali.

Badala ya kusimangwa kwa kuteleza maishani, wasichana hao wanafaa kupewa matumaini, ushauri nasaha na maelekezo ili waendelee na masomo.

Wazazi au walezi wao wanafaa kutumia wito wa serikali kuwapa motisha ili waendelee na kukamilisha elimu yao.

Enzi ambazo wasichana, na wanawake kwa jumla, walichukuliwa kama viumbe dhaifu zimepita.

Kuteleza kwa wanafunzi hao wa kike sio mwisho wa masomo wala maisha. Wanafaa kushikwa mikono na wasaidiwe kuinuka tena.

Wazazi na walimu kwa kushirikiana na viongozi wa kidini wawasaidie mabinti hawa kurekebisha palipoharibika na kuanza safari nyingine ya maisha.

Ni kweli kwamba kuwepo kwa wanafunzi walio na mimba shuleni ni changamoto sugu kwa wasimamizi sababu wana mahitaji ya kipekee yanayofaa kushughulikiwa kwa umakini.

Hata hivyo, hii ni gharama ambayo serikali inafaa kuwa tayari kubeba kwani wasichana hao ni sehemu ya jamii.

Tunatumia pesa nyingi kuwatunza washukiwa wa uhalifu wakizuiliwa rumande, baadhi yao wakiwa ni raia wa kigeni.

Hivyo kugharimikia wasichana wetu ili wapate usaidizi na kukamilisha elimu yao, ni mzigo tunaofaa kubeba bila kulalamika.

Inatia moyo kuona mashirika ya kijamii yameanzisha vituo maalumu kuwapa elimu wasichana hao ili waepuke unyanyapaa katika shule za kawaida.

Vituo kama hivyo vinafaa kuungwa mkono kikamilifu kwa kutengewa pesa katika bajeti kupitia Wizara ya Elimu.

Wizara pia inafaa kuanzisha vituo kama hivyo kote nchini ili wasichana wajawazito walio na kiu ya elimu waweze kunufaika.

Wakiwa katika vituo hivyo, watakuwa na mazingira bora ya kusoma huku wakishauriwa na kushughulikia watoto wao bila kuona aibu kwa kile kinachosemwa kuwahusu.

Itakuwa bora pia wanafunzi wavulana wakishauriwa katika juhudi za kuepuka mimba hizi za mapema.

Mara nyingi juhudi hizo zimekuwa zikielekezwa kwa mtoto msichana peke yake; wakati umewadia kuhusisha wavulana kikamilifu katika kila hatua.

Habari zinazohusiana na hii