• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
Bayern Munich wakomoa Tigres UANL na kutwaa Kombe la Dunia

Bayern Munich wakomoa Tigres UANL na kutwaa Kombe la Dunia

Na MASHIRIKA

BEKI Benjamin Pavard, 24, alifungia Bayern Munich bao la pekee lililosaidia Bayern Munich ya Ujerumani kupiga Tigres UANL ya Mexico 1-0 na kutwaa ufalme wa Kombe la Dunia kwa Klabu kwenye fainaili iliyochezewa nchini Qatar mnamo Alhamisi usiku.

Ushindi huo uliwezesha Bayern kutia kibindoni taji lao la sita chini ya kipindi cha miezi tisa iliyopita.

Bayern wametawazwa mabingwa wa Uefa Super Cup, German Super Cup na kwa sasa ndio wafalme wa dunia, ufanisi ambao umewashuhudia wakitwaa jumla ya mataji matatu kwa mpigo baada ya kunyanyua makombe mengine matatu katika kampeni za msimu uliopita wa 2019-20.

Awali, bao la Pavard lilikuwa limefutiliwa mbali na refa kwa madai ya kwamba alikuwa ameotea kabla ya maamuzi hayo kubatilishwa baada ya kurejelewa kwa video ya VAR.

Goli la Joshua Kimmich wa Bayern lilikataliwa baadaye a VAR katika mchuano huo uliotawaliwa na hisia kali. Hii ni baada ya kubainika kwamba alicheka na nyavu za Tigres wakati ambapo Robert Lewandowski alikuwa ameotea.

Ni mara ya nane mfululizo kwa Kombe la Dunia kwa Klabu kutwaliwa na kikosi kinachoshiriki soka ya bara Ulaya. Ubingwa wa mwaka uliopita wa 2020 ulinyakuliwa na Liverpool ambao kwa sasa ni watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Tigres ndiyo klabu ya kwanza kutoka Kaskazini na Amerika ya Kati kuwahi kutinga fainali ya Kombe la Dunia. Hata hivyo, walishindwa kukomesha ukiritimba wa vikosi vya bara Ulaya na Amerika Kusini kwenye vita vya kuwania ufalme wa taji hilo.

Licha ya kutofunga bao dhidi ya Bayern, mshambuliaji matata raia wa Ufaransa, Andre-Pierre Gignac alitawazwa Mfungaji Bora wa fainali za mwaka huu nchini Qatar baada ya kufuma wavuni jumla ya mabao matatu.

Kocha wa zamani wa Bayern, Pep Guardiola ambaye kwa sasa anadhibiti mikoba ya Manchester City nchini Uingereza, alirekodi video akiwapongeza masogora wa Bayern ambao kwa sasa wanatiwa makali na mkufunzi Hansi Flick.

“Hongereni sana familia pana ya Bayern kwa mafanikio yenu hayo makubwa. Nawastahi sana kwa juhudi zenu kwa sababu ni fahari kubwa na jambo la kipekee kutwaa jumla ya mataji sita kati ya sita chini ya kipindi cha miezi tisa,” akasema Guardiola kwenye video hiyo.

“Ningependa kumkubusha Flick kwamba Bayern sasa ndiyo timu ya pili baada ya Barcelona kutwaa mataji sita mfululizo katika historia ya soka duniani. Barcelona waliwahi kufanya hivyo mnamo 2009 chini ya Guardiola. Pengine sasa nimpigie Lionel Messi simu awatafute wenzake ili kucheza gozi la kuwania taji la saba mfululizo. Niambie ni lini na ni wapi gozi hilo litasakatwa,” akatania Guardiola ambaye ni raia wa Uhispania.

Qatar walikuwa wenyeji wa fainali za mwaka huu ili kupata fursa ya kufanyia majaribio baadhi ya vifaa na viwanja vitakavyotumika kuandalia fainali za Kombe la Dunia kwa mataifa mnamo 2022. Asilimia ndogo ya mashabiki walikubaliwa kuhudhuria fainali kati ya Bayern na Tigres katika uwanja wa Education City jijini Al Rayyan.

Ushindi kwa Bayern uliendeleza ubabe wao wa mwaka jana uliowawezesha kutawazwa Klabu Bora ya Mwaka 2020 baada ya kunyanyua jumla ya mataji matatu yakiwemo ya German Cup, Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Tangu Flick apokezwe mikoba ya Bayern mnao Novemba 2019, kikosi hicho kimeshinda jumla ya mechi 58 kutokana na 68. Ina maana kwamba miamba hao wamekuwa wakinyanyua taji kila baada ya kupiga wastani wa michuano 11.3.

Mbali na Pavard, Kimmich na Lewandowski, wanasoka wengine wa Bayern waliotatiza pakubwa mabeki na kipa wa Tigres ni viungo Leroy Sane na Corentin Tolisso aliyeaminiwa kuwa kizibo cha Leon Goretzka aliyepata jeraha wakati wa nusu-fainali dhidi ya Al Ahly ya Misri.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

MATHEKA: Serikali inafanya vyema kuwafaa wanafunzi...

Rupia aibuka mchezaji bora wa Desemba ligini