• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 8:55 AM
Tutakuwa tumedhibiti kero ya nzige kufikia Juni 2021 – Munya

Tutakuwa tumedhibiti kero ya nzige kufikia Juni 2021 – Munya

Na SAMMY WAWERU

WAZIRI wa Kilimo Bw Peter Munya amesema huenda taifa likawa limedhibiti kero ya nzige kufikia Juni 2021.

Bw Munya amesema serikali inaendelea kuimarisha mikakati kukabiliana na wadudu hao waharibifu.

Kulingana na mikakati iliyowekwa, alisema huenda nzige wakawa wamedhibitiwa kufikia mwezi wa Juni mwaka huu.

“Tunatarajia kuwa tumewakabili kufikia Juni 2021, kwa mujibu wa mipango na mikakati tuliyoweka,” akasema.

Waziri Munya alitoa hakikisho hilo baada ya kutembelea makao ya Shirika linaloangazia Masuala ya Mifugo Nchini (DVS), eneo la Uthiru, Kabete.

Waziri wa Kilimo Peter Munya (kati) akiwa katika makao makuu ya Shirika linaloangazia Masuala ya Mifugo Nchini (DVS), lililoko eneo la Uthiru, Kabete, ambapo alitumia jukwaa la ziara hilo kuhakikishia taifa serikali inafanya kila iwezalo kukabiliana na kero ya nzige. Picha/ Sammy Waweru

Alisema serikali imetengea oparesheni ya kukabiliana na nzige kima cha Sh3.2 bilioni.

“Tunashirikiana na Benki ya Dunia kuona tumekabili kero ya nzige,” akasema.

Mkurupuko wa makundi ya nzige nchini uliripotiwa mapema 2020.

Kufikia sasa, kaunti 15 zimethibitisha kuvamiwa na wadudu hao waharibifu.

Kaunti hizo zinajumuisha Mandera, Wajir, Garissa, Samburu, Isiolo, Marsabit, Meru, Tharaka Nithi, Tana River, Kilifi, Kitui, Laikipia, Nakuru, Nyandarua na Machakos.

Wakulima katika maeneo hayo wanaendelea kukadiria hasara kutokana na uharibifu wa mimea na mazao uliosababishwa na nzige.

Waziri Munya hata hivyo alisema serikali itapiga jeki walioathirika kwa kuwapa chakula cha msaada.

“Hatutawaachilia kuhangaika, tutawasaidia kwa chakula na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi,” akasema.

Nzige waliovamia maeneo yaliyoathiri wametajwa kuwa wadudu waharibifu, ambapo wakiingia kwenye shamba lenye mimea na mazao wanayala bila kusaza.

You can share this post!

Rupia aibuka mchezaji bora wa Desemba ligini

Hatimaye Samsung Galaxy S21 Ultra yaingia katika soko la...