• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Fasili ya lugha kama nyenzo ya kimsingi ya mawasiliano

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Fasili ya lugha kama nyenzo ya kimsingi ya mawasiliano

Na MARY WANGARI

KATIKA makala hii, tutaendeleza uchambuzi wa lugha kama kiungo cha kimsingi katika mawasiliano ya binadamu.

Lugha ni mfumo wa ishara – Hii inaashiriwa na jinsi maneno katika lugha huhusishwa au kuambatanishwa na hisia, mawazo, vitu, matendo yanayooana kwa njia ya unasibu.

Maandishi kwa mfano ni mkusanyiko wa ishara ambao maana yake inaweza kupatikana tu katika muktadha wa mawasiliano husika.

Ndiposa katika ujifunzaji lugha, ni sharti mwanafunzi afahamu mfumo na kanuni za lugha husika ikiwemo kuelewa uhusiano kati ya ishara zinazotumika na vitu vinavyowakilishwa.

Lugha hutumia sauti – Sauti inayotokana na ala za sauti ndiyo sifa kuu ya lugha katika mawasiliano.

Ala za sauti zinajumuisha sehemu mbalimbali za kinywa kama vile midomo, ulimi na sehemu zake mbalimbali, meno, kaakaa ya juu na ya chini, na kadhalika.

Maendeleo ya sayansi na teknolojia, yamewezesha binadamu kupiga hatua kubwa katika nyanja ya mawasiliano ikiwemo uandishi, tafsiri, matumizi ya lugha kimitambo, miongoni mwa mengine, ambapo sauti ndiyo kiambajengo kikuu.

Sauti ina dhima ya kimsingi katika lugha na mawasiliano kwa kuzingatia kuwa:

Tofauti kati ya lugha ya kuzungumza (sauti) na maandishi

Binadamu hujifunza lugha tangu utotoni mwake hata kabla ya kuanza kujifunza kusoma na kuandika.

Uelewa wa lugha kwa mtoto huwa ni wa moja kwa moja na huzidi kuimarika kadri mtoto anavyokua pamoja na mazingira yake.

Ni baada ya kujua kuzungumza ndipo mtoto anapojifunza kuandika herufi mbalimbali na kisha kujifunza kusoma.

Maandishi huwasilisha mazungumzo au mawasiliano yanayokusudiwa kupitishwa na mwandishi kwa hadhia lengwa.

Kwa kawaida, binadamu hutumia muda mwingi kuzungumza ikilinganishwa na kuandika.

Lugha ya kuzungumza au ukipenda sauti huweza kuashiria mambo mengi muhimu katika mawasiliano ambayo hayawezi kuwasilishwa au kujitokeza kisawasawa katika maandishi.

Baadhi ya mambo hayo ni kama vile: hisia, mkazo, kidato, kiimbo, toni, mkazo, kidatu.

Lugha ni kwa ajili ya mawasiliano – Ni lugha tu inayotofautisha binadamu na wanyama kwa kumwezesha kufanya mambo ambayo viumbe wengine hawawezi.

Lugha humwezesha binadamu kujieleza ikiwemo hisia zake, hofu, matarajio, shauku, matatizo na mengineyo kupitia kuzungumza tu, kuimba, kucheza kufanya kazi na kadhalika.

[email protected]

You can share this post!

Hatimaye Samsung Galaxy S21 Ultra yaingia katika soko la...

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Sifa bainifu za lugha kama...