• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Jinsi madiwani wanavyotishwa kupitisha BBI

Jinsi madiwani wanavyotishwa kupitisha BBI

Na BENSON MATHEKA

JUHUDI za kubadilisha Katiba kupitia Mchakato wa Maridhiano (BBI) zimechukua mkondo mpya na hatari, huku wanaouunga mkono wakitumia vitisho na nguvu kuhakikisha mabunge ya kaunti yamepitisha mswada ulioidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Haya yalibainika Alhamisi polisi waliporushia madiwani wa Bunge la Baringo vitoa machozi, katika kile kinachochukuliwa kuwa juhudi za kuwazuia kukataa mswada huo.

Kizaazaa kilizuka kwenye ukumbi wa mijadala wa bunge la kaunti hiyo polisi waliporusha gesi ya kutoa machozi muda mfupi baada ya madiwani kupigia kura mswada huo.

Madiwani walikuwa wametulia spika atangaze matokeo baada ya mjadala mkali uliokumbwa na vurumai, wakati polisi waliporusha gesi na kuwafanya watimke mbio.

Hatua hii ilijiri siku chache baada ya katibu mkuu wa chama cha Jubilee Raphael Tuju kukutana na madiwani wa bunge la kaunti ya Baringo jijini Nairobi kuwaagiza waunge mswada huo.

Baadaye, Bw Tuju aliotoa taarifa akionya madiwani wa chama hicho watakaokataa kuupitisha mswada huo watachukuliwa hatua.

Kwenye barua kwa viongozi wa wengi katika mabunge ya kaunti katika ngome za Jubilee, Bw Tuju alisema kwamba serikali itawaadhibu madiwani watakaokataa kuunga mswada huo.

Kulingana na Bw Tuju, itakuwa kukaidi uamuzi wa viongozi wa chama kwa madiwani wa Jubilee kukataa kuunga mkono mswada huo ambao una mengi mazuri ya kuwafaidi na kuwataka waunge msimamo wa chama kuhusu mswada huo.

Ijumaa, Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe aliunga kauli ya Bw Tuju akisema kwamba madiwani wa kaunti ya Baringo waliokataa kupitisha mswada huo wataadhibiwa.

Lakini mbunge wa Soy Caleb Kositany ambaye ni Naibu Katibu wa chama hicho na mshirika mkuu wa Naibu Rais William Ruto, aliwakosoa Murathe na Tuju akisema madiwani hawawezi kuadhibiwa kwa kutekeleza majukumu yao.

“Madiwani wa Baringo walithibitisha kwamba ruzuku ya Sh2 milioni ni haki yao lakini sio hongo. Wamekosa wabunge wa kuadhibu sasa wanaadama madiwani,” Bw Kositany alisema.

Alipokutana na madiwani wa eneo la Mlima Kenya kwenye ikulu ndogo ya Sagana wiki mbili zilizopita, Rais Uhuru Kenyatta aliahidi madiwani kwamba watapatiwa Sh2 milioni za kununua magari katika juhudi za kuwarai wapitishe mswada huo.

Wadadisi wanasema matumizi ya polisi kuvuruga shughuli katika bunge la kaunti ya Baringo kuzuia matokeo ya kura kuhusu mswada huo yanaonyesha kwamba wanaopigia debe mchakato wa kubadilisha katiba wanatumia vitisho kuhakikisha umepitishwa.

Wanasema kuna hofu kwamba huenda mabunge mengi ya eneo la Bonde la Ufa yakakosa kupitisha mswada huo.

Mswada huo unafaa kupitishwa na mabunge 24 ya kaunti ili kura ya maamuzi iweze kufanyika. Tayari mabunge ya Siaya, Kisumu na Homa Bay, ambazo ni ngome za chama cha ODM, yameupitisha bila kupingwa.

Wadadisi wanasema kwamba kilichotokea Baringo ni ujumbe kwa madiwani wa mabunge mengine kwamba hawatarajiwi kukataa kupitisha mswada huu.

Tayari mahakama imeagiza IEBC kutoandaa kura ya maamuzi kabla ya kesi saba za kuipinga kuamuliwa.

You can share this post!

Muuzaji wa dhahabu feki apatikana mashtaka ya kujibu

Kibwana, spika kupokea maoni kuhusu BBI