FATAKI: Unyenyekevu si udhaifu wala haupunguzi hadhi au nafasi yako kama mwanamume

Na PAULINE ONGAJI

WIKI iliyopita kulikuwa na mjadala kwenye kikundi kimoja kwenye mtandao wa kijamii ambapo baadhi ya wanachama walikuwa wakizungumzia hatua ya jamaa mmoja ya kuchapisha taarifa mtandaoni kumuomba mkewe msamaha.

Alitaja jina la mkewe na kusema kuwa alikuwa anaomba radhi kwa kumkosea kwa mambo mengi. Japo hakutaja kosa lake haswa, maneno yake yalionekana kuwa ya kweli na kutoka moyoni.

Japo kwa baadhi ya mabinti hatua ya mwanamume huyo ilikuwa ya kishujaa, kwa baadhi ya akina kaka walimuona kuwa dhaifu. Nakumbuka bwana mmoja akisema hatua hiyo ilishusha hadhi ya wanaume katika jamii. “Tangu lini mwanamume akakiri kosa hasa mbele ya mwanamke?”aliuza kwa mshangao.

Nakubaliana na baadhi ya maoni ya akina kaka kuwa msamaha unapaswa kutoka moyoni na sio jambo la kuwatangazia wengine, lakini bwana huyu apaswa kuigwa na wanaume humu nchini ambao kwao kusema pole ni hatia. Kuna baadhi ya wanaume wanaodhani kwamba unapoomba msamaha, basi hiyo ni ishara ya udhaifu. Hawaelewi kuwa mabinti wengi hutulizwa na hilo neno pole hasa wanapokosewa.

“Pole bibi nimekukosea”; “samahani bibiye nitachelewa kuja nyumbani leo”; “pole mpendwa nilisahau maadhimisho ya siku yako ya kuzaliwa” na kadhalika. Ingawa kwa baadhi ya madume wengi huo ni upuuzi, ni mambo yanayoongeza penzi na heshima katika uhusiano.

Tatizo na madume wengi hasa hapa nchini ni kuwa wamejawa na kiburi cha kudhani kuwa wao ni bidhaa adimu. Wafahamu kuwa vipusa wanataka kuonyeshwa penzi hadharani kwa kushikwa mkono mnapovuka barabara, kufunguliwa mlango, kumuacha aiingie mbele yako kwenye matatu na hata kumpa kiti iwapo hakuna nafasi kwenye gari.

Lakini mambo haya hayawezekani miongoni mwa baadhi ya mahambe hawa ambapo ni kawaida kung’ang’ania nafasi na mademu hata wajawazito kwenye matatu. Mambo haya ni mageni kwa baadhi yao kwani hawaoni hata haya kumtusi binti au hata kumshambulia na kumvua nguo eti kwa “kutovalia kiheshima”.

Madume waliomkejeli kaka huyu kwa kuonyesha tabia ya kingwana wanapaswa kuelewa kuwa dunia ya sasa inahitaji wanaume mfano huu; madume walio na unyenyekevu na roho nyepesi. Hii ni hasa ikiwa tunawataka mabinti wetu pia kunyenyekea. La sivyo, basi wajitayarishe kuzidi kupokonywa vipusa na wenzao kutoka Afrika Magharibi.

pongaji@ke.nationmedia.com

Habari zinazohusiana na hii