Ruto akwamilia ndoa ya machozi

Na JUMA NAMLOLA

NAIBU Rais William Ruto ameonekana kung’ang’ania kudumu kwenye ndoa ya kisiasa yenye mateso, kwa kutangaza kuwa ataendelea kumtumikia Rais Uhuru Kenyatta hata kama amempunguzia majukumu.

Akizungumza mjini Isiolo alikoongoza mchango wa kusaidia zaidi ya makanisa 70, Dkt Ruto alidai Jumamosi kuwa kutokana na heshima aliyo nayo kwa Rais Kenyatta, hatashindana naye kwa kuwa ndiye mwenye usemi wa mwisho.

“Hakuna mashindano kati yangu mimi na Rais wa Kenya. Yeye ndiye mkubwa wetu, tunamheshimu. Nyinyi mnajua mimi ni mtu wa heshima. Yeye ndiye mwenye kusema kwenye hii serikali. Na sijawahi kusema kinyume ya rais kwa sababu ya heshima. Hata kama kazi ninayopaswa kufanya inafanywa na wengine, mimi pia nimeheshimu uamuzi huo,” akasema.

Dkt Ruto akionekana kupuuza wito wa rais Kenyatta kwamba kama ameshindwa kutulia serikalini ajiondoe, alidai kuwa hajawahi kumpuuza Rais na amekuwa akifanya kila anachoagizwa.

“Mimi nafanya kazi ile ambayo Rais ameniambia nifanye. Hakuna kazi hata moja ambayo rais ameniambia nifanye na sijafanya,” akasema.

Mnamo Ijumaa, Rais Kenyatta alimwambia Dkt Ruto na wandani wake wajiuzulu badala ya kukosoa serikali wakiwa ndani.

Akizungumza akiwa Uthiru, Nairobi alipofungua hospitali mpya iliyojengwa na Idara ya Kusimamia jiji la Nairobi (NMS) na mradi wa maji, Rais Kenyatta alimlaumu Dkt Ruto na wandani wake kwa kuendelea kukosoa serikali ilhali wanataka kuendelea kuwa ndani.

“Tunafaa kushirikiana au kutengana. Iwapo wanahisi kwamba serikali inawafaa, basi wanastahili kushirikiana nasi lakini ikiwa wanataka kujitenga nayo, basi wajiuzulu,” Rais alisema.

Licha ya rais kuagiza wanasiasa kusitisha kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022, Dkt Ruto amemkaidi na kuendelea kujipigia debe akidai BBI inalenga kumzuia kugombea urais.

Lakini Jumamosi, Dkt Ruto aliwalaumu viongozi wa Upinzani kwa kauli hiyo ya Rais Kenyatta.

“Mimi nawaambia wale walikuwa wa upinzani wa zamani, wawache kuja kutuletea kisirani. Na wawache kuja kutuletea makasiriko. Huwezi kusema unashirikiana na sisi na kisha unauliza wapi laptop…” akasema Dkt Ruto.

Ingawa Wakenya walitarajia kuwa angejibu moja kwa moja kauli ya Rais, Dkt Ruto alionekana kusikiza ushauri wa wanasiasa alioandamana nao, ambao walimtaka asiingie kwenye mtego huo.

Tangazo lake kwamba ataendelea kumwamilia serikalini, huenda linatokana na Katiba kusema Rais hana mamlaka ya kumfuta kazi naibu wake ilivyokuwa katika katiba ya zamani.

Kipengele cha 150 cha katiba kinasema kwamba, naibu rais anaweza kuondolewa afisini akipata matatizo ya akili au kupitia mswada bungeni kwa misingi ya utovu wa nidhamu, kukiuka katiba au sheria yoyote ile na kutenda uhalifu chini ya sheria za Kenya na za kimataifa.

Habari zinazohusiana na hii

Uhuru aomba talaka

Watermelon mpya?

BBI: Ruto atapatapa

Mambo yaenda segemnege