• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
UDA yapigwa jeki uchaguzi Matungu

UDA yapigwa jeki uchaguzi Matungu

Na SHABAN MAKOKHA

MMOJA wa wagombeaji wa ubunge katika eneo la Matungu, Kaunti ya Kakamega, amejiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho na kutangaza kumuunga mkono mwaniaji wa chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Bw Anzelimo Kongoti, aliyekuwa akiwania kama mgombea wa kujitegemea alitangaza kuchukua hatua hiyo baada ya kufanya kampeni kwa muda wa mwezi mmoja.

Alitangaza kumuunga mkono Bw Alex Lanya, anayewania kiti hicho kwa tiketi ya UDA.

Bw Kongoti ndiye mwaniaji wa kwanza aliyeidhinishwa kuwania nafasi hiyo na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kujiondoa na kutangaza kumuunga mkono mgombea mwenzake.

Wawaniaji wengine waliokuwa wametangaza kugombea lakini wakajiondoa katika hali tatanishi kabla ya kuidhinishwa na IEBC ni Mabw Ernest Akeko, Nahashon Odanga na Arnold Maliba.

Bw Maliba alijiondoa kimya kimya, ingawa alionekana akiwa amepigwa picha pamoja na Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna. Baadaye, alitangaza kujiondoa.

Kiti hicho kiliachwa wazi mnamo Novemba 14, 2020, kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa eneo hilo, Justus Murunga.

Wenyeji wamekuwa wakidai wawaniaji hao walijiondoa baada ya “kununuliwa kisiasa”.

Wawaniaji walioamua kujiondoa kumuunga mkono Bw Lanya walidaiwa kupelekwa kukutana na Naibu Rais William Ruto, ambapo baadaye walitangaza hadharani kuchukua hatua hiyo.

Dkt Ruto anahusishwa na chama cha UDA ambacho nembo yake ni wilbaro.

Alhamisi iliyopita, Bw Kongoti alikutana na Dkt Ruto katika makazi yake mtaani Karen, jijini Nairobi, ambapo aliandamana na Waziri wa zamani wa Michezo, Rashid Echesa. Alitangaza kujiondoa baada ya kikao hicho.

Bw Kongoti alihudumu kama meya wa zamani wa Mumias.

“Leo, nilikutana na Bw Ronald Kongoti, ambaye alikuwa akiwania ubunge katika eneo la Matungu. Nilifanikiwa kumrai kujiondoa na kumuunga mkono mwaniaji wa mrengo wa ‘Hasla’, Alex Lanya,” akasema Dkt Ruto, kwenye ujumbe alioweka kwenye Twitter.

Hatua ya Bw Kongoti kujiondoa imepunguza idadi ya wawaniaji huru hadi wanane, huku wale wanaowania kwa tiketi za vyama mbalimbali vya kisiasa wakiwa sita.

 

Anzelimo Kongoti. Picha/ Maktaba

Wawaniaji wa kujitegemea ni Mabw Bernard Wakoli, Athman Wangara, Eugene Ambwere, Gregory Atoko, Kevin Neto, Wilberforce Lutta, Stanslaus Munyekenye na Bi Christabel Amunga, ambaye ni mkewe Bw Murunga.

Mbali na Bw Lanya, wale wanaowania kwa tiketi za vyama vya kisiasa ni Peter Nabulindo (ANC), David Were (ODM), Charles Kasamani (UDP), Auma Faida (Maendeleo Chap Chap) na Paul Achayo (MDG).

Mwezi uliopita, wawaniaji huru sita walialikwa jijini Nairobi na maseneta wa zamani Johnstone Muthama (Machakos) na Boni Khalwale (Kakamega), ambao ndio kiongozi na naibu kiongozi wa UDA mtawalia.

Wawaniaji hao walikataa rai za wanasiasa hao kujiondoa kinyang’anyironi ili kumuunga mkono Bw Lanya.

You can share this post!

Kinaya cha Sudi, Ng’eno katika jopo la nidhamu

Uganda yarukia EU kwa kutaka iwekewe vikwazo