• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 5:39 PM
JAMVI: Azma ya Mukhisa Kituyi kuwania urais pigo kwa Mudavadi

JAMVI: Azma ya Mukhisa Kituyi kuwania urais pigo kwa Mudavadi

SHABAN MAKOKHA Na BENSON MATHEKA

HATUA ya Mukhisa Kituyi kujiunga na kinyang’anyiro cha urais mwaka wa 2022 inaweza kupunguza nafasi ya kiongozi wa chama cha Amani National Congresss ( ANC), Musalia Mudavadi ya kumrithi Rais Uhuru Kenyatta ambaye atastaafu baada ya kuhudumu kwa mihula miwili.

Bw Kituyi alijiuzulu kama katibu wa Shirika la biashara na ustawi la Umoja wa Mataifa (UNCTAD) majuzi na anatarajiwa kurejea nchini Februari 15 kuanza kampeni zake za kugombea urais.

Amehudumu katika Umoja wa Mataifa tangu Septemba 1 2013 kwa mhula wa miaka minne ambao uliongezwa muda 2017.

Mbunge huyo wa zamani wa Kimilili na wakati mmoja waziri wa biashara na viwanda alikatiza kandarasi yake ikibakia miezi kadhaa kukamilika kugombea urais nchini kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Mapema 2020 Kituyi, 65, alitangaza kuwa ameiva kuwa rais wa Kenya kufuatia tajiriba yake katika jukwaa la kimataifa.

“Sio siri tena. Niko tayari na nitagombea urais mwaka wa 2022 kwa sababu kuna pengo la uongo katika nchi hii na inahitaji rais atakayekomboa uchumi wetu usioporomoke,” Bw Kituyi aliambia Taifa Jumapili akiwa Matungu.

Aliwahimiza Wakenya kutofautisha mbinu za kisiasa kutoka malengo ya siasa akisema watu wengi wanaonyesha mbinu badala ya malengo yao ya kisiasa.

“Yeyote anayetaka kuwa rais ni lazima aeleze Wakenya kwa nini anataka kuingia mamlakani, hii inafaa kuwa kutatua shida za Wakenya na kuwapa matumaini kwa kuimarisha uchumi,” alisema.

Tangazo lake linaonekana kama pigo kwa Bw Mudavadi ambaye anachukuliwa kuwa msemaji na mbabe wa siasa eneo la Magharibi.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa Martin Andati, kujitosa kwa Bw Kituyi kwenye kinyang’anyiro cha urais, kutamfanya Bw Mudavadi kuongeza nguvu zaidi kuimarisha umaarufu wake na kuunganisha eneo la Magharibi nyuma yake.

“Asiketi na kufikiri kwamba anamiliki watu wa eneo la Magharibi na hakuna mwingine anayeweza kupenya huko. Hii itamfanya Mudavadi kuzinduka na kuwekeza katika azima yake. Asipoongeza juhudi Mukhiya atampiku kwa umaarufu,” asema Andati.

Hata hivyo, anasema Dkt Kituyi atalazimika kuzunguka Kenya kueleza Wakenya atakachowafanyia.

“Itategemea uzito wa atakachowaambia Wakenya, ndicho kitamfanya kuwa mgombeaji mwenye nguvu au akose kuvuma. Ikiwa ataweza kumwangusha Mudavadi na Wetangula eneo la Magharibi basi atakuwa mbabe wa kisiasa eneo hilo. Lakini iwapo atashindwa kuwabandua, atazimika kujiunga nao ili wakubaliane watakavyoshirikiana,” alieleza Andati.

Mdadisi huyu anasema ni lazima Bw Kituyi aliandaa mikakati yake vyema mashinani kabla ya kujiuzulu kutoka kazi yenye mshahara mnono ya Umoja wa Mataifa.

“Lazima kuna mambo kadhaa aliyozingatia kabla ya kufanya uamuzi kwa sababu hakuna anayeweza kuamka siku moja na kuamua kujiuzulu kutoka kazi anayolipwa zaidi ya Sh10 milioni kwa mwezi kucheza kamari ya kutaka urais,” alisema Andati.

Anasema kwa kuwa Kituyi anatoka jamii ya Wabukusu kunampatia alama zaidi katika azima yake ya urais kwa kuwa jamii hiyo inachangamkia siasa ikilinganishwa na jamii nyingine za jamii pana ya Mulembe.

“Bw Kituyi ni mwanasiasa aliyepevuka, mwanaharakati na mtu aliyesoma anayeelewa anachotaka katika maisha. Sio mtu unayeweza kupuuza hivi hivi,” asema.

Kulingana na mwanasiasa mmoja ambaye aliomba tusifichue jina lake kwa kuwa sio msemaji wa mwanasiasa huyo, Dkt Kituyi amerejea Kenya na kwamba katika muda wa wiki mbili zijazo, ana mipango kabambe.

“Alijiuzulu kutoka wadhifa wake katika Umoja wa Mataifa na amerudi akiwa na ujumbe ambao utafuatiwa na kampeni kali,” alisema.

Kitui amerudi nchini leo Jumapili.

Alifichua kwamba kuna mikutano mikubwa ambayo itakuwa ya kumpigia debe Bw Kituyi kote nchini.

Wakati wa mazishi ya Bi Hannah Mudavadi katika kijiji cha Mululu, Kaunti ya Vihiga, Rais Uhuru Kenyatta aliashiria kuwa huenda wakati umefika wa mtu kutoka jamii ambazo hazijatoa rais kuongoza nchi.

Kauli hiyo ilichangamkiwa na viongozi wa ANC ambao walidai kwamba Rais alikuwa amemuidhinisha Bw Musalia Mudavadi kumrithi akiondoka mamlakani 2022.

Lakini kulingana na Bw Andati, alichomaanisha rais ni kuwa hangetaka kukabidhi uongozi mtu kutoka jamii za Wakikuyu na Wakalenjin.

“Ilikuwa makosa kwa viongozi wa ANC kufikiria kwamba Rais Kenyatta alimaanisha mtu kutoka nje ya Wakikuyu na Wakalenjin alikuwa Mudavadi. Anaweza kuunga yeyote kutoka jamii 40 zilizobaki,” alisema.

Baadhi ya wadadisi wanasema kwamba si ajabu Rais Kenyatta akamuunga Bw Kituyi kwa sababu anatoka nje ya jamii hizo mbili.

Rais Kenyatta akimuunga Bw Kituyi, Mudavadi atakuwa amepata pigo kubwa kwenye azima yake ya kuwa rais wa tano wa Kenya kwa kuwa kulingana na mbunge wa Lugari Ayub Savula, makamu rais huyo wa zamani anasubiri rais kumuidhinisha kuwa mrithi wake.

Hata hivyo, Bw Mudavadi amesisitiza kuwa hatarajii kuidhinishwa na yeyote isipokuwa wapigakura kwenye uchaguzi ili aweze kuingia Ikulu.

You can share this post!

Napoli wazamisha Juventus kwenye Serie A na kuokoa kazi ya...

Kaunti yagawa kondomu 100,000