• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
DINI: Siku njema huonekana asubuhi, ijaze dua na kuichangamkia kwa furaha

DINI: Siku njema huonekana asubuhi, ijaze dua na kuichangamkia kwa furaha

Na FAUSTIN KAMUGISHA

SIKU njema huonekana asubuhi, ni methali ya Kiswahili.

Atakayekula vizuri chakula anatambulika wakati wa kunawa mikono, ni methali ya Tanzania.

Mwanzo unakupa mwelekeo. Asubuhi inakupa mwelekeo wa siku. Saa ya asubuhi ni rada ya siku. Saa ya asubuhi ni kifungua mimba cha neema za siku.

“Asubuhi ndipo mtakapouona utukufu” (Kutoka 16:7).

Ndege anayeamka asubuhi na mapema ndiye anapata mnyoo. Anza siku na Mungu.

“Wale ambao wanamkimbia Mungu asubuhi ni mara chache sana kumpata wakati mwingine wa siku,” alisema John Bunyan. Saa ya asubuhi ni mlango wa siku.

“Asubuhi ni lango la siku na lilindwe vizuri kwa sala. Asubuhi ni mwisho mmoja wa uzi ambapo matendo ya siku yanafungwa, fundo lake lifungwe vizuri kwa ibada. Kama tunahisi utukufu wa maisha, tuwe makini na asubuhi zake,” alisema Robert D. Foster.

Asubuhi ni wakati kati ya kuchomoza kwa jua na kabla ya kuanza adhuhuri.

“Saa ya asubuhi ni dhahabu mkononi,” alisema Benjamin Franklin.

Kuna hadithi ya watu watatu waliokuwa wanasafiri kwenye jangwa. Walisikia sauti ikiwaambia: “Okota mawe madogo madogo myaweke mifukoni. Kesho asubuhi mtazame kwenye mifuko yenu.”

Hawakutilia maanani maneno hayo. Hivyo, waliokota mawe kidogo sana. Kesho yake walipotazama katika mifuko yao walifurahi sana na walisikitika sana.

Walifurahi sana maana mawe hayo yalibadilika na kuwa madini ya thamani sana-dhahabu.

Walisikitika sana maana waliokota kidogo. Walifanya kosa la kutookota mawe mengi.

Uliyoweza kujipatia jana, ukiamka asubuhi hayo ni dhahabu mkononi. Kama jana ulishindwa kutumia wakati vizuri inasikitisha asubuhi.

Kupata fursa ya kuamka salama, ni dhahabu. Kupata fursa ya kupumua na kuvuta hewa, ni dhahabu. Kupata fursa ya kufikiri asubuhi, ni dhahabu.

“Maisha yanaanza kila asubuhi! Kila usiku wa maisha ni ukuta kati ya leo na jana. Kila asubuhi ni mlango wazi wa dunia mpya, mandhari mpya, malengo mapya, kujaribu tena upya,” alisema Leigh Mitchell Hodges.

Dunia mpya ya asubuhi ni dhahabu. Mandhari mapya ni dhahabu. Malengo mapya ni dhahabu.

“Asubuhi panda mbegu zako.” (Mhubiri 11:6). Panda mbegu za mawazo chanya, mipango endelevu na kuwekeza.

Ichangamkie kila asubuhi kama asubuhi yako ya kwanza duniani. Ijaze shukrani, dua, maombi na maombezi. Ijaze hamasa, furaha, matumaini, upendo na ukarimu. Ijaze na mpango kazi wa siku.

Kila asubuhi ni baraka kutoka kwa Mungu. Unaweza kufanya mambo matano. Kwanza, amka asubuhi na mapema. Jua lisikukute kitandani.

Pili, sali. “Sala ni ufunguo wa asubuhi na komeo la jioni,” alisema Mahatma Gandhi.

Tatu, fanya mazoezi. “Zoezi la kutembea asubuhi na mapema ni baraka kwa siku yote,” alisema Henry David Thoreau.

Nne, soma maandiko matakatifu na vitabu vya kutia moyo.

Tano, fanya kazi kama kuandika au kazi nyingineyo.

Siku ya Papa Francis inaanza saa 10.30 asubuhi. Kabla ya saa 11 asubuhi anakuwa ameamka. Anatumia masaa mawili yanayofuata kusali, kusoma Neno la Mungu na kuandaa homilia ya asubuhi.

Billionea wa Marekani, Bill Gates, hulala saa 6 usiku na kuamka saa 1 asubuhi.

Aliko Dangote, mtu tajiri sana katika Afrika mwenye utajiri wa dola 11.2 billioni kulingana na jarida la Forbes, huanza siku yake saa 11 asubuhi.

Anafanya mazoezi anapoamka. Kuhusu mazoezi alisema, “Mazoezi ni mazuri zaidi ya dawa yoyote ambayo naweza kuchukua.” Yeye hulala masaa manne au matano lakini usingizi mzito.

Nelson Mandela katika kitabu chake “A Long Walk to Freedom” alieleza jinsi alikuwa akiamka saa 10.30 alfajiri.

Baraka Obama mwaka 2009 alielezea ratiba yake kama rais wa 44 wa Marekani. Alikuwa na haya ya kusema, “Mimi ni bundi wa usiku. Siku yangu ya kawaida iko hivi: Naenda ofisini kati ya saa 2.30 hadi 3.00 asubuhi; nafanya kazi hadi saa 12.30 jioni. Napata chakula cha usiku na familia na kuongea na watoto kabla kuwaweka kitandani saa 2.30.

Baadaye nasoma muhtasari wa magazeti au kufanya kazi ya vitabuni au kuandika mpaka saa 5.30, halafu nakuwa na nusu saa ya kusoma.”

Yote tisa, ukweli unabaki kuwa maisha ni muda, uutumie vizuri.

You can share this post!

Kaunti yagawa kondomu 100,000

Mradi wa serikali wa kurembesha jiji wageuzwa eneo la...