• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 4:28 PM
EPRA: Atwoli aitaka wizara husika ajitokeze kumtetea raia wa kipato cha chini

EPRA: Atwoli aitaka wizara husika ajitokeze kumtetea raia wa kipato cha chini

Na CHARLES WASONGA

KATIBU Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi Nchini (COTU) Francis Atwoli ameitaka wizara husika iingilie kati ongezeko la bei ya mafuta kwa kiwango kikubwa akisema asipofanya hivyo, wafanyakazi wataathirika zaidi na hatua hiyo.

Kwenye taarifa kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter Bw Atwoli amesema nyongeza ya bei iliyotangazwa na Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi Nchini (EPRA) pia itawaathiri zaidi wananchi wanaokabiliwa na hali ngumu ya uchumi kipindi hiki cha janga la Covid-19.

“Ni vibaya na ishara ya kutojali kwa EPRA kuruhusu nyongeza ya bei ya hadi Sh8.19, Sh5.51 na Sh5.32 mtawalia kwa kila lita ya petroli, dizeli na mafuta ya taa. Hatua kama hii inachochea kupanda kwa bei ya bidhaa za matumizi kote nchini na gharama ya usafiri ambapo wafanyakazi ndio wataathirika pakubwa kupitia ongezeko la nauli,” Bw Atwoli akaeleza.

Alaongeza: “Tunataka wizara husika kuingilia kati suala hili mara moja kwa kubatilisha nyongeza ya bei ya mafuta jinsi ilivyotangazwa Jumapili, Februari 14.”

Atwoli amesema EPRA inapaswa kuchukua hatua ya haraka kuzuia kile alichotaja kama makabiliano kutoka kwa wafanyakazi na Wakenya wanaopitia “hali ngumu wakijaribu kuweka chakula mezani tangu kulipuka kwa janga la corona mwaka 2020.”

Kupanda huko kwa bei ya mafuta sasa kunamaanisha kuwa bei ya rejareja ya petroli jijini Nairobi itapanda hadi Sh115.18 kutoka Sh107 kwa lita, dizeli itauzwa kwa Sh101.91 kutoka Sh96.8 huku mafuta taa yakiuzwa Sh92.44 kutoka bei ya zamani ya Sh87.78.

Bei hizi zitaaanza kutekelezwa usiku wa manane. Bei ya mafuta katika miji mingine nchini itakuwa tofauti kulingana na umbali wake kutoka mji wa Mombasa ambako mafuta hushuka kutoka ng’ambo.

“Bei hiyo inajumuisha ushuru wa VAT wa asilimia nane jinsi ilivyopendekezwa katika Sheria ya Fedha, 2018, Sheria ya Mabadiliko ya sheria za Ushuru, 2020 na kusawazishwa kwa ushuru mwingineo na kiwango cha mfumkobei,” EPRA ikasema Jumapili kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.

Mamlaka hiyo imeongeza kuwa kupanda huko kwa bei ya mafuta, kwa kiwango kikubwa, kumechangiwa na kupanda kwa bei ya mafuta ghafi aina ya Murbane katika masoko ya kimataifa.

Katika mwezi wa Januari bei hiyo ilipanda hadi dola 55.27 (Sh6,500) kwa pipa moja kutoka dola 49.57 (Sh5,660) mnamo Desemba 2020. Hii ni sawa na ongezeko la bei la kima cha asilimia 11.50.

Katika kipindi hicho sarafu ya Kenya iliongezeka thamani kutoka Sh110.5 kwa dola moja ya Amerika mnamo Desemba 2020 hadi Sh109.89 kwa dola. Kiwango hicho ni sawa na kuimarika kwa sarafu ya Shilingi ya Kenya kwa kima cha asilimia 0.57.

You can share this post!

Moise Kean afungia PSG tena na kuwaongoza kutua kileleni...

COVID-19: Kenya yathibitisha visa vipya 75