• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:24 AM
COVID-19: Kenya yathibitisha visa vipya 75

COVID-19: Kenya yathibitisha visa vipya 75

Na CHARLES WASONGA

HAKUNA mgonjwa aliyethibitishwa kufariki kutokana na Covid-19 Jumapili, huku Kenya ikiendelea kuandikisha idadi ndogo ya visa vipya vya maambukizi.

Hii ina maana kuwa idadi jumla ya watu waliofariki kutokana na homa hii ingali imesalia kuwa 1,795.

Kulingana na taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Wizari ya Afya Mutahi Kagwe watu wengine 75 walipatikana na virusi vya corona baada ya sampuli kutoka watu 3,025 kupimwa ndani ya saa 24 zilizopita.

Visa hivyo vipya vilipatikana kutoka kaunti zifuatazo; Nairobi iliandikisha visa 51 ikifuatwa na Kiambu iliyorekodi visa sita. Nayo kaunti ya Busia iliripoti visa vine (4), Uasin Gishu (2) , Mombasa (2), Nyeri (2) huku kaunti za Garissa, Homa Bay, Kirinyaga, Meru, Murang’a, Nakuru, Nyandarua, na Trans Nzoia, kila moja ikirekodi kisa kimoja cha maambukizi.

“Wakati huo huo, jumla ya wagonjwa 56 wamepona na kuruhusiwa kurejelea maisha yao ya kawaida. 37 walikuwa wakiuguzwa nyumbani huku 19 wakiwa ni wale ambao walikuwa wamelazwa katika hospitali mbalimbali,” akasema Waziri Kagwe.

Hii ina maana kuwa idadi jumla ya wagonjwa waliopona tangu mwaka 2020 sasa ni 85,008.

Kulingana na Waziri Kagwe wagonjwa 347 sasa wamelazwa katika katika hospitali mbalimbali nchini wakiugua Covid-19 huku wengine 1,275 wakiuguzwa chini ya mpango wa utunzwaji nyumbani.

“Wagonjwa 33 wamelazwa katika vyumba vya kuwahudumia wagonjwa mahututi (ICU), 18 kati yao wakiwa ni wale wanaosaidiwa kupumua kwa mitambo ya ‘ventilators” huku wengine 18 wakiongezwa hewa ya oksijeni,” taarifa hiyo ikaeleza.

You can share this post!

EPRA: Atwoli aitaka wizara husika ajitokeze kumtetea raia...

Wolves wang’ata Southampton na kupaa kwenye jedwali...