• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 6:47 AM
Maangi na Osoro wakamatwa katika mazishi ya Nyachae

Maangi na Osoro wakamatwa katika mazishi ya Nyachae

Na SAMMY WAWERU

Mbunge wa Mugirango Kusini, Bw Silvanus Osoro na Naibu Gavana wa Kisii Joash Maangi wamekamatwa na maafisa wa polisi katika hafla ya mazishi ya Mzee Simeon Nyachae inayoendelea katika uga wa Gusii, Kaunti ya Kisii.

Kulingana na idara ya polisi, Osoro amezuiwa kushiriki mazishi hayo ambayo yamehudhuriwa na Rais Uhuru Kenyatta, Naibu wa Rais, Dkt William Ruto na kinara wa ODM, Bw Raila Odinga kwa tuhuma za kuwa na mipango kuzua rabsha.

Naye Bw Maangi alanaswa katika Shule ya Upili ya Kisii ambapo alikuwa ameenda kupokea wageni, na kupelekwa kwa afisi za DCI.

Bw Maangi ndiye sauti ya Naibu Rais Dkt William Ruto katika kaunti za Kisii na Nyamira.Bw Osoro ambaye pia ni mwandani wa karibu wa Dkt Ruto anadai “kukamatwa kwangu kunachochewa kisiasa”.

Akithibitisha kukamatwa kwa Osoro, msaidizi wake Bw Joseph Oriango amesema hawajui anakopelekwa mbunge huyo.

Idara ya polisi hata hivyo imesema inataka kumhoji zaidi kuhusu madai ya kuzua fujo.

Kutiwa nguvuni kwa mbunge huyo kumejiri saa chache baada ya Naibu Gavana wa Kisii, Bw Joash Maangi kukamatwa mapema Jumatatu kwa sababu zisizoeleweka.

Duru zinasema Bw Maangi alitiwa pingu na maafisa wa polisi katika Shule ya Upili ya Kisii High, wakati akijiandaa kumkaribisha Naibu wa Rais.

Februari 1, 2021, katika mazishi ya Mzee Abel Gongera (babake Maangi), Osoro na mbunge wa Dagoretti, Simba Arati waliangushiana makonde katika hafla hiyo ambayo ilihudhuriwa na Dkt Ruto na Bw Raila Odinga.

Familia ya Mzee Simeon Nyachae imeomba viongozi na wanasiasa waliohudhuria mazishi ya mwendazake, kutogeuza hafla ya kumpa heshima za mwisho kuwa ukumbi wa cheche za siasa na matusi.

You can share this post!

BBI yaunganisha vigogo wa Mulembe

Buriani Mzee Simeon Nyachae