Buriani Mzee Simeon Nyachae

Na SAMMY WAWERU.

MWANASIASA mkongwe Mzee Simeon Nyachae amezikwa Jumatatu nyumbani kwake katika kijiji cha Nyosia, Kaunti ya Kisii.

Rais Uhuru Kenyatta, Naibu wake, Dkt William Ruto na kinara wa ODM, Bw Raila Odinga ni kati ya viongozi ambao wamehudhuria hafla hiyo ya mazishi, kumpa mwendazake heshima za mwisho.

Wengine ni kiongozi wa ANC, Bw Musalia Mudavadi, kiongozi wa KANU, Seneta Gedion Moi, miongoni mwa wengine, pamoja na viongozi wakuu serikalini na wanasiasa.

Bw Nyachae aliaga dunia Februari 1, 2021 akiwa na umri wa miaka 88.

Alihudumu kwenye nyadhifa mbalimbali katika serikali ya Rais Mzee Jomo Kenyatta (babake Rais wa sasa Uhuru Kenyatta) na ambaye ni marehemu, Rais Daniel Arap Moi ambaye pia ni marehemu na Rais Mstaafu Mwai Kibaki.

Mwaka wa 1960, Bw Nyachae alihudumu kama Mkuu wa Wilaya katika Divisheni ya Kangundi.

Mwendazake alistaafu kutoka utumishi wa umma 1987, akaanza kujijenga kisiasa.

Mwaka wa 1992, alijiunga na ulingo wa siasa ambapo alichaguliwa mara ya kwanza kama mbunge wa Nyaribari Chache, na Rais Moi akamteua kuwa Waziri wa Kilimo.

Aidha, alichaguliwa kwa tiketi ya chama cha KANU. Nyadhifa zingine alizohudumu ni pamoja na Waziri wa Fedha na Waziri wa Ustawi.

Baadaye, alijiuzulu na kugura KANU, akajiunga na chama pinzani katika utawala wa Moi, Ford-People.

Mwaka wa 2002, Bw Nyachae alikataa kujiunga na muungano wa National Rainbow Coalition (NARC) ambao ulihusisha chama cha LDP kilichoongozwa na Raila Odinga, DP cha Mwai Kibaki, kati ya vyama vingine vikuu.

Aliwania urais, ingawa akabwagwa na Rais Kibaki. Rais wa sasa Uhuru Kenyatta pia aliwania urais kwa tiketi ya chama cha KANU.

Mwaka wa 2004, Rais Kibaki alimteua Bw Nyachae kuwa Waziri wa Nishati na baadaye Barabara, kufuatia mgawanyiko wa kisiasa ulioanza kushuhudiwa ndani ya NARC.

Katika uchaguzi mkuu wa 2007, Nyachae hakufua dafu kuhifadhi kiti chake cha ubunge.

Mzee Nyachae ndiye baba ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Utekelezaji Katiba (CIC), Bw Charles Nyachae.

Kando na kuwa mwanasiasa, Mzee Nyachae pia alikuwa mfanyabiashara mashuhuri.