• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 2:16 PM
KDF yashangazwa na makurutu kuwa na vyeti vyenye majina tofauti

KDF yashangazwa na makurutu kuwa na vyeti vyenye majina tofauti

RICHARD MAOSI NA ALICE KARIUKI

MAAFISA wa kusajili makurutu kwenye Jeshi la Kenya (KDF) Kaunti ya Nakuru Jumatatu walishangazwa na vyeti vya vijana wengi waliojitokeza kuwa na majina tofauti.

Mamia ya vijana walijitokeza kwenye uwanja wa Shule ya Upili ya Kampi ya Moto, eneo la Rongai kushiriki katika zoezi la kujiunga na KDF, lakini ukosefu wa uwiano wa majina katika vyeti vyao vya Kuzaliwa, Vitambulisho, KCPE na KCSE ukawafungia nje.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali, Mkuu wa Kitengo cha Kusajili Makurutu(SRO), Kanali Luteni Dennis Obiero, alifichua kuwa stakabadhi za vijana wengi hazikuwa na majina sawa.

“Tunawahimiza vijana kurekebisha vyeti vyao mapema ili kuhakikisha kuwa wanashiriki katika zoezi la kujiunga na jeshi bila matatizo,”akasema.

“Hii ni kuhakikisha kuwa shughuli nzima inaenda sambamba na masharti ya kujiunga na kikosi cha jeshi”

Aidha aliwaomba vijana kutahadhari na matapeli ambao, huitisha pesa wakidai wana uwezo wa kuwaunganisha na kikosi, akidai kuwa ni hatia na ingeweza kumtumbukiza mhusika katika matatizo.

Visa vya ukosefu wa uwiano wa majina kwenye stakabadhi viliripotiwa. Picha/Richard Maosi

“Ikiwa mtu hatafaulu kujiunga na jeshi sio mwisho wa dunia, ila anaweza kutumia fursa hiyo kujiongezea masomo katika taasisi za kiufundi na kupanua tajriba itakayomfaa baadaye katika zoezi kama hili mwaka ujao 2022,” aliongezea.

Wakati wa zoezi vijana walijipanga kulingana na maeneo wanayotoka, hatimaye utaratibu wa kukagua vyeti na stakabadhi za masomo ulifuata.

Hatima yeke ilikuwa ni kuchunguza alama ya vidole , kuhakikisha sura yake ni sawa na ile ya kitambulisho.

Kutoka hapo walikaguliwa miguu, uzani, urefu, meno na kushiriki kwenye mbio ya kilomita tano. Uchunguzi zaidi wa damu na washiriki wenye stakabadhi bora wakapatiwa kipaumbele.

Isitoshe kanuni za kuzingatia msambao wa corona zilishuhudiwa huku washiriki wakipimwa joto na kusafisha mikono, kabla ya kuingia uwanjani

Hafla kama hii ilifanyika katika kaunti ndogo za Gilgil na Njoro, zoezi zima likitarajiwa kukamilika Jumanne wiki hii katika uwanja wa Nakuru Showground(ASK)

You can share this post!

Buriani Mzee Simeon Nyachae

Wanaharakati waitaka serikali kupiga marufuku matumizi yote...