• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
Wanaharakati waitaka serikali kupiga marufuku matumizi yote ya plastiki

Wanaharakati waitaka serikali kupiga marufuku matumizi yote ya plastiki

NA KALUME KAZUNGU

WANAHARAKATI wa mazingira, Kaunti ya Lamu wanaishinikiza serikali kupiga marufuku matumizi ya vyombo vya plastiki nchini ili kuzuia uchafuzi wa mazingira na kuhatarisha viumbe hai.

Wakizungumza baada ya kukusanya tani zaidi ya 20 za plastiki, wanaharakati hao chini ya mwavuli wa wakfu wa Taka Taka, walieleza hofu yao kuhusiana na ongezeko la chupa, mirija na vyombo vingine vya plastiki ambavyo kila kukicha vinarushwa kiholela baharini na kwenye fuo mbalimbali eneo hilo.

Msemaji wa Wakfu wa Taka Taka, Ali Skanda, alisema njia ya kipekee kwa Kenya kuwa huru dhidi ya athari na kero la plastiki ni kuhakikisha marufuku inaanzishwa ya matumizi ya aina hiyo ya vyombo nchini.

Bw Skanda alisema licha ya Kenya kuamuru marufuku kuanzishwa dhidi ya matumizi ya mifuko ya plastiki kote nchini tangu Agosti, 2017, changamoto ya kukithiri kwa uchafu wa plastiki bado ipo kote Kenya.

“Tunaishukuru serikali kwa kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya platiki nchini lakini hatua hiyo bado haitoshi. Plastiki bado imejaa tele baharini, ufuoni na kwenye miji yetu. Ipo haja ya aina yoyote ya chombo cha platiki kupigwa marufuku Kenya iwapo tungependa kuwa na mazingira huru yasiyokuwa na athari wala kero la plastiki,” akasema Bw Skanda.

Naye Bw Abdul Baabad, alishikilia kuwa ipo haja ya wanajamii kuhamasishwa kuhusiana na athari za plastiki ili kuepuka kurusha ovyo taka hizo.

Msemaji wa wanaharakati wa mazingira Lamu, Ali Skanda akionyesha takataka zilizokusanywa za plastiki karibu tani 20 mjini Lamu. Picha/ Kalume Kazungu 

Alisema kupitia wakfu wa Taka Taka, wakazi wa Lamu wamekuwa wakishirikishwa kwenye harakati za kuokota na kukusanya uchafu wa plastiki na pia kupewa mafunzo na mbinu muhimu za jinsi watakavyotumia plastiki kwa njia salama.

Bw Baabad alisema licha ya marufuku ya wakenya kutii amri ya kutotumia mifuko ya plastiki nchini, aina nyingine ya plastiki, hasa chupa na mirija bado ni kero kwa mazingira hasa yale ya baharini.

“Sisi kama wakfu wa Taka Taka tumekuwa tukiwashirikisha n ahata kuwahamasisha wananchi jinsi watakavyojizuia kuchafua kiholela mazingira kupitia plastiki. Tayari tumekusanya zaidi ya tani 20 za plastiki kutoka fuo mbalimbali za bahari Lamu. Haya yote tunayafanya ili kuwahamasisha wananchi jinsi plastiki zinavyoathiri mazingira yetu ili waepuke kufanya hivyo. Cha msingi aidha ni serikali kuzuka na marufuku ya matumizi ya plastiki zote kote nchini,” akasema Bw Baabad.

Ali Shebwana aliitaka serikali kuu na ile ya kaunti kupitia idara ya Afya ya Umma kuandaa makongamano ya mara kwa mara ili kuwaelimisha wananchi kuhusiana na umuhimu wa mazingira safi bila plastiki.

Bw Shebwana aidha alieleza wasiwasi wake kuhusiana na ongezeko la uchafu wa glasi zinazotumiwa kutengeneza boti na mashua na kisha kutupwa ovyo kwenye fuo za bahari hindi Lamu.

“Ningeomba kaunti, serikali kuu na Shirika la Mazingira (NEMA) kuanda worsha za mara kwa mara kuelimisha umma juu ya kutunza mazingira,” akasema Bw Shebwana.

You can share this post!

KDF yashangazwa na makurutu kuwa na vyeti vyenye majina...

Makuhani wa usaliti