• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:23 PM
Mazishi yageuka rungu la kuchapa Ruto

Mazishi yageuka rungu la kuchapa Ruto

WYCLIFFE NYABERI na WANDERI KAMAU

MAZISHI ya waziri wa zamani, Bw Simeon Nyachae, Jumatatu yaligeuka kuwa uwanja wanasiasa kumponda Naibu Rais William Ruto katika kile kilichoonekana kama ushindani wa siasa za uchaguzi wa 2022.

Baadhi ya viongozi waliohutubu kwenye mazishi hayo yaliyofanyika katika Uwanja wa Gusii, walitumia mafumbo kumshambulia vikali Dkt Ruto, wakimlaumu kwa kuonyesha kiburi na kuwakumbusha Wakenya kuhusu wadhifa wake.

Kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi, alisema licha ya kuwa na mamlaka makuu na ushawishi wa kisiasa, Bw Nyachae daima alionyesha unyenyekevu mkubwa.

“Sifa kuu ambayo marehemu alionyesha ni unyenyekevu. Ilikuwa vigumu kujua ushawishi aliokuwa nao kisiasa na kibiashara. Alionyesha uwezo wake kwa vitendo wala si majisifu,” akasema Bw Mudavadi katika mazishi hayo ambayo viongozi wengine kama vile Rais Uhuru Kenyatta na waziri mkuu wa zamani Raila Odinga walijiepusha na kauli za kisiasa.

Seneta Gideon Moi wa Baringo naye alisema inawezekana mtu kufanikiwa maishani bila kutumia wizi ama uporaji wa mali ya umma.

“Nyachae alikuwa mfanyabiashara maarufu aliyetumia bidii na jasho lake. Hakutumia njia za mkato kupata mali aliyokuwa nayo,” akasema Bw Moi, ambaye pia ndiye mwenyekiti wa Kanu na mshindani wa Dkt Ruto katika siasa za Bonde la Ufa.

Kauli hizo zilionekana kumlenga Dkt Ruto ikizingatiwa kuwa amekuwa akisisitiza ndiye Naibu Rais wa Kenya licha ya changamoto ambazo zimekuwa zikimwandama. Wawili hao ni wapinzani wa kisiasa wa Dkt Ruto.

Maswali yamekuwa yakiibuka kuhusu kiasi halisi cha utajiri wake, kutokana na michango mikubwa ambayo amekuwa akitoa kwenye hafla za harambee.

Dkt Ruto amekuwa akihusishwa na kashfa za ufisadi, baadhi zikiwa kandarasi tata za ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer, inakodaiwa serikali ilipoteza zaidi ya Sh21 bilioni.

Mazishi hayo pia yaligeuka kuwa siku ndefu kwa Naibu Gavana wa Kisii Joash Maangi na mbunge Sylvanus Osoro (Mugirango Kusini) baada yao kukamatwa na kuzuiwa kuhudhuria mazishi hayo. Wawili hao ni washirika wa karibu wa Dkt Ruto.

Kwenye hafla hiyo, Rais Kenyatta, Bw Odinga, Bw Mudavadi, Bw Kalonzo Musyoka (Wiper) na wengine waliongoza maelfu ya waombolezaji kuipa pole familia.

Kila aliyepata nafasi ya kuhutubu hakusita kummiminia sifa Mzee Nyachae kwa ukakamavu aliouonyesha alipokuwa akihudumu serikalini na alipoingia kwenye siasa. Rais Kenyatta alimkumbuka Mzee Nyachae kwa ushauri wake nasaha aliopata kutoka kwake. Aliahidi jamii ya Abagusii ushirikiano wake anapoendeleza shughuli za kuliongoza taifa.

Rais alitaja kifo cha Nyachae kuwa pigo kwa taifa na kusema Kenya itazikosa huduma za kiongozi huyo.

Mbali na kumsifu Bw Nyachae, Bw Odinga alidokeza kuwa hakumuunga mkono alipokuwa akiwania urais katika uchaguzi wa 2002, kwani alihisi wawili hao hawangeshinda kwenye uchaguzi huo hata kama wangeungana.

Dkt Ruto alisimulia jinsi Mzee Nyachae alivyomfanya apoteze kiatu chake akiwa kwenye kampeni eneo la Kisii.

Alisema hajasahau ukali wa Mzee Nyachae alipomuadhibu yeye na aliyekuwa Mbunge wa Mugirango Kusini, Omingo Magara.

“Licha ya tofauti ya umri kati yangu na Mzee Nyachae, kama alivyosema Charles (Nyachae), tulikuwa na uhusiano. Kijana wake Michael aliposoma wasifu wa mzee alisema alikuwa mtu mkali, aliyetekeleza sheria hata kwa kiboko. Michael aliogopa kutaja waliokumbana na kiboko hicho kwa sababu jina langu lingekuwamo kwenye orodha,” akasema Dkt Ruto.

Alisimulia kisa cha mwaka 2007, katika eneo la Nyamarambe, ambapo alilazimika kukimbilia kwenye helikopta akiwa na kiatu kimoja mguuni.

“Nakumbuka vyema Nyamarambe, mimi na Omingo Magara tulikosa adabu. Na Michael hakusema kwa sababu yeye ndiye mtu aliyetumwa na Mzee Nyachae akachukue kiboko. Na hapo, tulipata…kuadhibiwa.”

You can share this post!

IMF kukopesha Kenya Sh262b kufufua uchumi

Wambora ailaumu Serikali kwa kudhalilisha wakulima