Mwenyekiti wa BBI azikwa bila cheche za siasa

Na WANDERI KAMAU

RAIS Uhuru Kenyatta jana aliungana na maelfu ya Wakenya kumuaga Seneta wa Garissa, Yusuf Haji, aliyefariki na kuzikwa jana katika makaburi ya Lang’ata, Nairobi, kulingana na kanuni za dini ya Kiislamu.

Bw Haji alihudumu kama seneta wa Garissa kuanzia 2013, ambapo pia ndiye alikuwa mwenyekiti wa jopo la Mpango wa Maridhiano (BBI).

Kiongozi wa ODM, Raila Odinga, pia alikuwa miongoni mwa viongozi waliofika kwenye makaburi hayo.

Bw Haji alifariki jana wakati akipokea matibabu katika Hospitali ya Aga Khan, Nairobi.

Kwenye ujumbe wake wa rambirambi, Rais Kenyatta alimtaja Bw Haji kuwa kiongozi mkakamavu, mzalendo na aliyetegemewa kusimamia masuala muhimu yanayoihusu nchi.

“Mzee Haji alikuwa kiongozi aliyeheshimika, ambaye tajriba na maarifa yake vilimwezesha kuitumikia nchi katika nyadhifa mbalimbali kwa ukakamavu mkubwa,” akasema Rais.

Naibu Rais William Ruto alimtaja kama afisa wa utawala aliyekita utendakazi wake kwenye malengo aliyokusudia kuyatimiza.

“Daima tutamkumbuka Mzee Haji kama kiongozi aliyekuza uadilifu katika utumishi wa umma,” akasema.

Bw Odinga alimtaja kuwa “kiongozi mzalendo na mtumishi wa umma mwenye unyenyekevu mkubwa.”

Viongozi wengine waliomwomboleza ni Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka, Spika wa Seneti Ken Lusaka, Spika Justin Muturi wa Bunge la Kitaifa kati ya wengine.

Kiongozi huyo alizaliwa mnamo Desemba 23, 1940 katika Kaunti ya Garissa (wakati huo ikiwa wilaya).

Anatoka kwenye koo ndogo ya Ogaden katika jamii ya Wasomali.

Alisomea katika Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingereza, alikopata Diploma katika Usimamizi wa Biashara na Masuala ya Kifedha.

Alijiunga na serikali mnamo 1960 na kuanza kuhudumu kama mkuu wa taarafa (DO). Baadaye, alipandishwa ngazi na kuwa Mkuu wa Mkoa (PC), alikohudumu kati ya 1970 na 1997.

Mnamo 1998, aliteuliwa kama mbunge maalum. Kati ya 1998 na 2001, alihudumu kama Waziri Msaidizi katika Afisi ya Rais. Baadaye, alipandishwa ngazi na marehemu Daniel Moi kuwa Waziri katika Afisi ya Rais hadi 2002.

Mnamo 2002, alichaguliwa kama mbunge wa eneo la Ijara kwa tiketi ya Kanu, ambapo alihudumu hadi 2007.

Aliteuliwa kuhudumu kama Waziri wa Ulinzi, Januari 2008, baada ya uchaguzi tata wa Desemba 2007. Alihudumu hadi Aprili 2013.

Kwenye uchaguzi wa 2013, aliwania Useneta katika Kaunti ya Garissa, ambako aliibuka mshindi kwa tiketi ya Muungano wa Jubilee.

Alishinda tena nafasi hiyo mnamo 2017, alikohudumu hadi kifo chake.

Mnamo Juni 18, 2012, Bw Haji aliteuliwa na Rais Mstaafu Mwai Kibaki kuhudumu kama Kaimu Waziri wa Usalama wa Ndani baada ya kifo cha Prof George Saitoti kwenye ajali ya ndege.

Haji alikuwa amefanya kazi kwa karibu na Prof Saitoti kwenye operesheni ya Linda Nchi, iliyolenga kuilinda mipaka ya Kenya dhidi ya kushambuliwa na magaidi.

Amewaacha watoto tisa, ingawa mmoja kati yao alifariki.

Miongoni mwa watoto wake ni Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP), Noordin Haji.

Habari zinazohusiana na hii

BBI YAINGIA ICU

Kwani kuliendaje?