BBI: Madiwani wataka kikao na Uhuru, Ruto

Na ONYANGO K’ONYANGO

MADIWANI kutoka eneo la Bonde la Ufa wanataka kukutana na Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto, huku kampeni kuhusu ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI), zikiendelea kushika kasi.

Eneo hilo ni ngome ya kisiasa ya Dkt Ruto. Madiwani walisema kuwa mkutano huo utasaidia pakubwa kuondoa taharuki iliyopo katika Chama cha Jubilee (JP), wakimlaumu Katibu Mkuu Raphael Tuju kuwa chanzo chake kikuu.

Tayari, madiwani kutoka kaunti za Elgeyo-Marakwet, Uasin Gishu, Nandi, Kericho na Bomet wamemwambia Bw Tuju kukoma kuingilia utendakazi wao.

Walisema kuwa kufikia sasa, hakuna msimamo wowote rasmi uliotolewa na chama kuhusu mchakato huo.

Kiongozi wa Wengi katika Kaunti ya Bomet, Bw Josphat Kirui, aliiambia Taifa Leo kwamba masuala yanayohusu mageuzi ya kikatiba hayahitaji uwepo wa masharti na maagizo bila pande husika kushauriana. Bw Kirui alisema masuala hayo yanapaswa kuwa maamuzi ya kibinafsi.

Alisema kuwa Jubilee inapaswa kuiga chama cha ODM, ambapo kiongozi wake, Bw Raila Odinga, aliwarai madiwani kuiunga mkono ripoti. Alieleza matumizi ya nguvu na vitisho yatazua taswira kama zilizoshuhudiwa kwenye Bunge la Kaunti ya Baringo, ambapo madiwani walikabiliana baina yao.

“Rais anapaswa kuwa na kikao maalum na viongozi wa Jubilee sawa na alivyoandaa mkutano maalum na madiwani kutoka ukanda wa Mlima Kenya. Anapaswa kumwiga Raila, kwa kukutana na madiwani na kuwaelezea faida za BBI badala ya kutumia nguvu kama anavyofanya Tuju,” akaeleza.

“Utoaji vitisho hautakuwa wenye manufaa yoyote. Bw Tuju anapaswa kujiepusha na mwelekeo huo, la sivyo huenda baadhi yetu tukafasiri uwepo wa njama fiche kwenye ripoti hiyo,” akaongeza.

Hata hivyo, Bw Kirui alisema watu wanapaswa kuondoa dhana kuwa mabunge yaliyo kwenye kaunti zinazomuunga mkono Dkt Ruto lazima ziuangushe mswada huo kwani ameeleza baadhi ya vipengele ambavyo haviungi mkono.

“Tumekutana na Dkt Ruto hapo awali lakini hakutwambia tuikatae BBI. Badala yake, kupitishwa kwake kutalingana na sababu tatu; ambazo ni jinsi itakavyoshughulikia ugatuzi, maslahi ya madiwani na maamuzi ya wananchi,” akasema.

Akaongeza: “Lazima tutenganishe mchakato huu na siasa za 2022.”

Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kaunti ya Kericho, Bw Hezron Ngetich, alisema chama hakijatoa msimamo rasmi kuhusu mswada huo, hivyo Bw Tuju anapaswa kukoma kutumia vitisho.

Alisema kuwa kama viongozi waliochaguiliwa, madiwani watafanya maamuzi yao kulingana na matakwa ya wananchi.

“Mwelekeo wa BBI katika ukanda huu utalingana na maamuzi yatakayotolewa na wananchi baada yao kushirikishwa,” akasema.

Madiwani waliozungumza na Taifa Leo walisema watazingatia matakwa ya wananchi wala hawatafuata maagizo ya viongozi wa kisiasa.

Habari zinazohusiana na hii

BBI YAINGIA ICU

Kwani kuliendaje?