• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
Pigo mabunge ya Kenya yakipoteza wabunge watano

Pigo mabunge ya Kenya yakipoteza wabunge watano

Na CHARLES WASONGA

JUMATATU, Februari 15, ilikuwa siku yenye mkosi kwa mabunge ya Kenya – Seneti na Bunge la Kitaifa – kufuatia vifo vya Seneta Mohammed Yusuf Haji na baadaye jioni Mbunge wa Bonchari John Oroo Oyioka akakata roho.

Saa moja baada ya Mzee Haji kuzikwa katika makuburi ya Waislamu ya Lang’ata, familia ya Bw Oyioka ilithibitisha kifo chake katika hospitali ya Aga Khan Kisumu ambako alikuwa amelazwa akipokea matibabu baada kuugua.

Mbunge huyo amekuwa akipokea matibabu kwa kipindi cha mwaka mmoja baada ya kuugua kiharusi kapema mwaka jana. Mapema mwaka huu alilazwa katika hospitali ya Aga Khan Kisumu ambako amekuwa akipokea matibabu.

Bw Oyioka, ambaye ni mwalimu wa miaka mingi, alijiunga na siasa mnamo 2013 ambapo aliwania kiti cha ubunge cha Bonchari.

Kwa bahati mbaya alikuwa wa pili katika uchaguzi huo ambapo alishindwa na Zebedeo Opore kwa kura tano pekee.

Aliwasilisha kesi katika Mahakama Kuu ya Kisii kupinga ushindi wa Opore aliyepata kura 8,992. Na katika uamuzi uliotolewa mnamo Septemba 2013, mahakama ilimtangaza Oyioka kuwa mshindi na kutoa nafasi kwake kuhudumu kama mbunge wa Bonchari.

Hata hivyo, alihudumu kama Mbunge kwa miezi sita pekee kwani Mahakama ya Rufaa iliagiza kufanyike uchaguzi mdogo ambapo Bw Opore alishinda kwa mara nyingine.

Hakukata tamaa kwani mnamo 2017, Bw Oyioka aliwania kiti hicho cha Bonchari na kuibuka mshindi kwa tiketi ya KANU iliyokuwa imeshirikiana na chama cha People Democratic Party (PDP) katika uchaguzi huo.

Kwa bahati mbaya amefariki kabla ya kukamilisha muhula wake wa miaka mitano na kujiunga na orodha ya wabunge ambapo wamefariki katika muhula huu wa Bunge la 12.

Wao ni Justus Murunga (Matungu), James Lusweti Mukwe (Kabuchai) na maseneta Boniface Mutinda Kabaka na Yusuf Haji.

Kando na kuhudumu kama Mbunge wa Bonchari, Marehemu Oyioka amekuwa mwanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Elimu ambapo alitoa mchango muhimu zaidi haswa kuhusiana na masuala ya utendakazi wa Wizara ya Elimu.

Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi amemuomboleza Oyioka kwa kumtaja kama mbunge ambaye alichukulia kwa uzito wajibu wake bungeni na katika kamati ya elimu alikohudumu.

“Kama bunge la kitaifa tunamkumba Mheshimiwa Oyioka kama mwanachama shupavu wa kamati ya elimu na ambaye alipigania kuimarishwa kwa ubora wa elimu kote nchini. Kwa niaba yangu na Bunge la Kitaifa natoa pole kwa familia na marafiki wa mwendazake,” akasema Bw Muturi

Gavana wa Kisii James Ongwae pia alielezea kuhunishwa na kifo cha Oyioka saa chache baada ya kaunti hiyo kumpa mkono wa buriani kigogo wa siasa za jamii ya Abagusii Simeon Nyachae.

“Rambi rambi zangu na maombi yaendee kaunti ya Kisii kwa ujumla familia, jamaa na marafiki wa mheshimiwa,” Ongwae akasema.

You can share this post!

Wakana kuiba Sh3.5 m, hela za mfu

Raila alimeza ‘tear gas’ ya Sh50m