• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 5:50 AM
Raila alimeza ‘tear gas’ ya Sh50m

Raila alimeza ‘tear gas’ ya Sh50m

Na WANDERI KAMAU

SERIKALI ilitumia zaidi ya Sh10 milioni kila mwezi kununua gesi ya kutoa machozi kuwakabili wafuasi wa kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, walioandamana jijini Nairobi kulalamikia matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanywa Agosti 2017.

Hayo yalielezwa jana na Katibu wa Usalama wa Ndani, Dkt Karanja Kibicho, aliyesema serikali ililazimika kuongeza bajeti yake kununulia gesi hiyo kuwawezesha polisi kuwatawanya waandamanaji.

Maandamano yalikuwa yakifanyika karibu kila wiki kuanzia Agosti, na yakatulia tu wakati Bw Odinga alipoingia muafaka wa maelewano na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Machi 2018.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio, Dkt Kibicho alisifia uwepo wa handisheki kati ya viongozi hao wawili, akisema fedha hizo sasa zimekuwa zikielekezwa kwa masuala mengine yanayohusu maslahi ya polisi.

“Hali ilikuwa ngumu kwani kabla ya handisheki tulikuwa tukitumia zaidi ya Sh10 milioni kila mwezi kununulia gesi ya kutoa machozi pekee kukabili maandamano. Hicho ni kiasi kikubwa cha fedha. Mambo ni tofauti sasa, kwani fedha hizo sasa zinatumika kushughulikia masuala mengine yanayohusu uboreshaji wa idara ya polisi,” akasema katika ufichuzi unaoonyesha kuwa zaidi ya Sh40 milioni zilitumika kwa jumla.

Baada ya matokeo ya uchaguzi wa urais mnamo 2017 kuonyesha Rais Kenyatta alimshinda Bw Odinga, wafuasi wa muungano wa Nasa waliapa kufanya maandamano jijini Nairobi kila Jumatatu kushinikiza mabadiliko katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).Maandamano hayo pia yalitokea katika ngome nyingine za Bw Odinga kama vile jiji la Kisumu.

Mbali na Bw Odinga, muungano huo uliwashirikisha kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, Bw Musalia Mudavadi (ANC), Seneta Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) na aliyekuwa gavana wa Bomet, Bw Isaac Rutto, anayeongoza Chama Cha Mashinani (CCM).

Kwenye maandamano hayo, yaliyoitwa Jumatatu ya Machozi (Machozi Mondays), Bw Odinga na viongozi wa Nasa walikuwa wakipiga kambi katika Jumba la Anniversary, ambalo ndilo makao makuu ya IEBC, wakishinikiza maafisa wake wakuu kujiuzulu.Hasa, walimlaumu aliyekuwa afisa mkuu mtendaji wa tume hiyo, Ezra Chiloba kwa “kupanga njama za kuwaibia kura kwa kushirikiana na Chama cha Jubilee(JP)”.

Muungano huo pia ulieleza kupoteza imani kwa uongozi wa mwenyekiti wa tume hiyo, Bw Wafula Chebukati, ukitaja hilo kuwa sababu kuu ya kutoshiriki kwenye marudio ya uchaguzi huo yaliyofanyika Oktoba 26, 2017.Kwa wakati mmoja, ilibidi walinzi wa Bw Odinga kumwokoa baada ya gari lake kurushiwa gesi na polisi walipopiga kambi katika jengo hilo na kuanza kuwahutubia wafuasi wake.

Akirejelea matukio hayo, Dkt Kibicho aliitaja ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) kuwa njia bora na ya pekee itakayohakikisha matukio kama hayo hayarejelewi tena nchini.

“Hatuwezi kuwaruhusu watu kadhaa kutuzuia kutekeleza mpango utakaohakikisha kuna amani hata baada ya uchaguzi kukamilika,” akasema.Wakati huo huo, katibu huyo alieleza kuwa kufikia sasa, serikali imechapisha nakala milioni 20 za ripoti hiyo, na “mipango inaendelea kuhakikisha zimewafikia wananchi.”

Alisema shughuli hiyo inaendelea katika Matbaa ya Serikali, na zitasambazwa baada ya wananchi kupewa mafunzo kamili kuhusu yale yaliyo kwenye ripoti hiyo.Wakenya katika sehemu mbalimbali nchini wamekuwa wakilalamika kuhusu kutofikiwa na nakala hizo.

You can share this post!

Pigo mabunge ya Kenya yakipoteza wabunge watano

Pwani yasisitiza itakaa ODM hadi mwisho, haitaunda chama