• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 2:55 PM
BBI sasa yafaulu kunasa kaunti za kwanza Bondeni

BBI sasa yafaulu kunasa kaunti za kwanza Bondeni

Na WAANDISHI WETU

MABUNGE ya kaunti za Pokot Magharibi, Busia na Trans Nzoia, Jumanne yalipitisha mswada wa kugeuza katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI), na kufikisha jumla ya mabunge yaliyoiunga mkono kuwa sita.

Madiwani wa bunge la Kaunti ya Pokot, wamekuwa wa kwanza katika eneo la Kaskazini mwa Rift Valley ambalo ni ng’ome ya Naibu Rais kupitisha mswada huo.

Dkt Ruto amekuwa akipinga mchakato huo. Wiki jana bunge la Kaunti ya Baringo lilikataa kuunga mswada huo.Baada ya kujadili mswada huo kwa muda wa saa mbili, madiwani wa Kaunti ya Pokot walisema kwamba waliupitisha kwa kuwa kaunti zitapata asilimia 35 ya mgao wa mapato na kaunti yao itapata maeneobunge mapya.

Mswada huo uliwasilishwa na kiongozi wa wengi, Bw Thomas Ngolesia na kuungwa na kiongozi wa wachache, Bw Peter Lokor.

Wote waliozungumza walisifu mswada huo wakisema unafaidi maeneo yaliyotengwa kama kaunti yao.Gavana wa kaunti hiyo, Prof John Lonyangapuo na mbunge wa Pokot Kusini, Bw David Pkosing, walihudhuria kikao hicho madiwani walipokuwa wakijadili mswada huo.

Nao madiwani wa Kaunti ya Busia, walipitisha mswada huo wakisema uliungwa na wakazi wa maeneobunge yote saba.Mswada huo ulijadiliwa na umma katika maeneobunge ya Nambale, Matayos, Budalang’i, Butula, Funyula, Teso Kusini na Teso Kaskazini kuanzia Februari 9 hadi 12.

Ni diwani mmoja kati ya 53 aliyepinga mswada huo ulipowasilishwa na mwenyekiti wa kamati ya sheria na haki za binadamu ya bunge la Kaunti ya Busia, Bw David Kokonya.

Kwingineko, viongozi wa kisiasa katika kaunti za eneo la Mlima Kenya, wameanza kampeni kali ya kushawishi wakazi watenganishe BBI na maazimio ya Bw Odinga na kuzingatia manufaa ambayo eneo lao litapata.

Msimamo huo ni sawa na aliochukua Bw Odinga alipohojiwa na kituo kimoja cha redio cha lugha ya Kikikuyu wiki mbili zilizopita, aliposema kwamba BBI hailengi kumsaidia kumrithi Rais Kenyatta kipindi chake cha mwisho kitakapomalizika.

Naibu Rais William Ruto na wandani wake huwa katika mstari wa mbele kuhusisha BBI na siasa za 2022, akidai ni njama ya Bw Odinga na wenzake kutaka kuingia mamlakani kwa urahisi.

Kampeni ya kuhakikisha mswada wa marekebisho ya katiba wa BBI utapitishwa eneo la Mlima Kenya zimeshika kasi baada ya kuwasilishwa katika baadhi ya mabunge ya kaunti na ushirikishi wa umma kuanza.

Shughuli hiyo itaendelea kwa siku kadhaa kabla ya mswada huo kurudishwa katika mabunge ya kaunti kujadiliwa na kupigiwa kura.Gavana wa Kaunti ya Tharaka Nithi, Bw Muthomi Njuki, alisema kwamba watu wengi eneo la Mlima Kenya wanapinga mswada huo hata baada ya kuelewa yanayopendekezwa wakifikiri yanalenga kumsaidia Bw Odinga kuwa rais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Alisema, hata mapendekezo hayo yakipitishwa, Wakenya watakuwa na haki yao ya kidemokrasia ya kuwachagua viongozi wanaowataka.

“Tunafaa kutenga BBI na Bw Odinga na uchaguzi wa 2022 na kuunga kwa sababu ni nzuri kwa nchi,” alisema.Mbunge wa Maara, Bw Kareke Mbiuki, aliwataka wanasiasa kukoma kupotosha Wakenya kwamba BBI inalenga kumnufaisha Bw Odinga.

Alisema badala ya kuingiza siasa katika BBI, wanasiasa wanafaa kuhakikisha imetafsiriwa kwa lugha tofauti na nakala kupatiwa Wakenya wote ili wajisomee.

Katika Kaunti ya Kirinyaga, Gavana Anne Waiguru, katika hotuba yake kwa Bunge la Kaunti Jumatano, alipigia debe mswada huo na akawahimiza madiwani wa Kirinyaga kutenganisha masuala ya BBI na uchaguzi mkuu wa 2022.

Naibu Spika wa bunge la Kaunti ya Embu, Bw Steve Simba, alithibitisha kwamba mipango ya kupitisha mswada huo imekamilika, akisema madiwani wengi wameahidi kuunga mkono mchakato wa kubadilisha katiba.

Bunge la Kaunti ya Tharaka Nithi, limebuni kamati inayoshirikisha madiwani wote kushughulikia mswada huo ambao uliwasilishwa na naibu spika, Bw John Njagi ambaye ni diwani wa wadi ya Chiakariga.Spika David Mbaya aliagiza kamati hiyo kuwasilisha ripoti yake ijadiliwe na kupigiwa kura ndani ya muda wa siku 30.

Katika Kaunti ya Nyeri, mswada huo uliwasilishwa katika bunge la kaunti na kiongozi wa wengi, Bw James Kanyugo.Spika John Kaguchia aliagiza kamati ya sheria kuujadili na akahimiza madiwani kutekeleza jukumu lao la kikatiba kuupitisha.

Mwenyekiti wa muungano wa madiwani wa eneo la Mlima Kenya, Bw Charles Mwangi, aliambia Taifa Leo kwamba watatii mwito wa Rais Kenyatta wapitishe mswada huo katika siku 30 zijazo.

“Hatutaki mabunge yetu ya kaunti kubadilika kuwa majukwaa ya vita vya kisiasa kati ya maslahi mbali mbali yaliyomo katika siasa za BBI. Hii ndiyo sababu tutapitisha mswada huo na kupitisha presha kwa bunge la kitaifa na seneti,” alisema.

Ripoti za Regina Kinogu, Alex Njeru, Waweru Wairimu, George Munene na Mwangi Muiruri, Oscar Kakai na Shaban Makokha

You can share this post!

Pwani yasisitiza itakaa ODM hadi mwisho, haitaunda chama

Yaibuka uwanja wa ndege hutegemea vibuyu kuchota maji