• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
CHARLES WASONGA: Wabunge wanaodaiwa kupokea hela za mafuta wachunguzwe

CHARLES WASONGA: Wabunge wanaodaiwa kupokea hela za mafuta wachunguzwe

Na CHARLES WASONGA

WAKATI huu ambapo Wakenya wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha, inavunja moyo kusikia kuwa wabunge wanatumia nafasi zao kuendeleza ufisadi serikalini.

Siku mbili kabla ya Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Petroli (EPRA) kupandisha bei ya mafuta kwa kiwango kikubwa mno, hatua ambayo itachochea kupanda kwa gharama ya maisha, wabunge walifichua sakata ya matumizi mabaya ya fedha za ushuru wa mafuta.

Kiongozi wa wachache, Bw John Mbadi alitoboa kwamba wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Kawi hupokea Sh50 milioni, kila moja, kutoka kwa hazina ya Ushuru wa Mafuta za kufadhili miradi katika maeneo bunge yao.

Mbunge huyu wa Suba Kusini aliungama kuwa fedha hizi hutolewa na Wizara ya Uchukuzi kwa wabunge hao 17 kama “zawadi kwa kazi wanazofanya za kutetea bajeti ya wizara hiyo na kufuatilia utendakazi wake.”

Alisema hayo wakati mjadala mkali uliibuka wakati wa kuidhinishwa kwa wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti.Swali langu ni je, mbona wabunge wanachama wa kamati hii wapewe sehemu ya fedha ambazo Wakenya wote hutozwa kama ushuru wa mafuta kama kiinua mgongo?

Ni miradi ipi hufadhiliwa kwa fedha hizo ilhali kila eneo bunge hupokea Sh137 milioni, kila mwaka, kutoka kwa Hazina ya Ustawi wa Maeneo Bunge?

Nashuku kuwa pesa hizi hufaidi wabunge husika wala si wananchi kwa sababu matumizi yazo huwa hayakaguliwi na Afisi ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali.

Huu ni ufisadi ambao unapaswa kuchunguzwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na wahusika waadhibiwe kwa mujibu wa sheria.

Inaudhi kwamba wakati ambapo mamlaka ya EPRA inasema kuwa mojawapo ya sababu zilizochangia kupandishwa kwa bei ya mafuta ni viwango vya juu vya ushuru unaotozwa bidhaa hiyo, baadhi ya wabunge wanafaidi kinyume cha sheria kwa fedha hizo.

Ni wajibu wa wabunge, haswa wanachama wa Kamati ya Kawi, kuhakikisha kuwa ushuru wa mafuta unatumiwa kukarabati barabara kote nchini.

Haifai wao kufaidi kubinafsi kutokana na fedha hizo zinazolipwa na Wakenya wanaopitia hali ngumu ya maisha haswa wakati huu wa janga la corona.

Uovu kama huu ambapo wabunge hufaidi kifedha kutokana kwa wizara na asasi ambazo wanapaswa kukagua utendakazi wazo, ni wa kukemewa. Spika Justin Muturi aliungama kuwa sakata hii inaendelea lakini akadai kuwa “wahusika ni wabunge wachache.”

Namhimiza kualika EACC iwachunguze wabunge hao “wachache” wanaoiharibia sifa asasi ya bunge ambayo inapaswa kuwa mtetezi wa umma.

You can share this post!

Pigo kwa chama cha UDA Machakos baada ya wandani kutoroka

SGR ya Kisumu kukamilika 2022