• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 3:23 PM
Waziri motoni kukodisha choo kwa Sh2.3m

Waziri motoni kukodisha choo kwa Sh2.3m

Na DAVID MWERE

WAZIRI wa Maji Sicily Kariuki ameagizwa kufika mbele ya wabunge kujibu maswali kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma alipohudumu kama Waziri wa Utumishi wa Umma na Masuala ya Vijana.

Miongoni mwa madai yaliyofichuliwa kwenye ripoti inayohusu matumizi ya fedha ni kuhusu ukodishaji wa choo uliogharimu Sh2.3 milioni, na utumizi wa helikopta iliyokodishwa na shirika la Huduma za Taifa kwa Vijana (NYS) kwa mambo ya kibinafsi, uliogharimu serikali Sh7.7 milioni.

Wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu (PAC) wanamtaka Bi Kariuki kutoa maelezo kuhusu matumizi hayo yaliyotambuliwa na afisi ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali katika wizara hiyo katika mwaka wa kifedha wa 2017/2018.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa kamati hiyo Opiyo Wandayi wakati wa ukaguzi wa matumizi ya fedha katika Wizara ya Utumishi wa Umma, wabunge hao waligundua kuwa Bi Kariuki, alitumia helikopta, iliyokodiwa na shirika la NYS kwa Sh7.7 milioni kuwasafirisha wafanyakazi, kwa shughuli zake za kibinafsi.

Helikopta hiyo ilimsafirisha kwa hafla ya kibinafsi katika mkahawa wa Windsor ulioko katika barabara ya Kiambu.Kamati hiyo pia ilielezwa kuwa Wizara hiyo ilitumia Sh2.3 milioni kukodi vyoo tamba kwa matumizi ya siku moja katika mkutano wa chama cha akiba na mikopo (sacco) ulioongozwa na Bi Kariuki katika Chuo cha Mafunzo ya NYS, Gilgil.

“Hili suala la ukodishaji wa vyoo tunavyoona ni haramu na linaashiria matumizi mabaya ya mamlaka na Waziri kwa sababu huu ulikuwa mkutano wa kibinafsi,” Bw Wandayi akasema huku akimwambia Katibu wa Masuala ya Vijana Mary Kimonye kumwacha Bi Kariuki abebe msalaba wake.”

Kutokana na hili, ni wazi kuwa Sicily Kariuki ambaye ndiye alikodi vyoo hivyo ndiye Waziri aliyetumia helikopta ya umma kwenda katika mkahawa wa Windsor,” Bw Wandayi akasema, akiongeza “tutamwagiza kufika mbele ya kamati hii ili tupambane naye.”

Suala la matumizi ya helikopta liliibuka baada ya ripoti ya ukaguzi wa matumizi ya fedha kufichua kuwa malipo yaliyotolewa yalijumuisha gharama ya safari ya kwenda Windsor, ilhali safari hiyo haikuidhinishwa na afisa husika.

Bw Wandayi alitaja jina la Bi Kariuki baada ya Bi Kimonye na Mkurugenzi Mkuu wa NYS Matilda Sakwa, ambao walifika mbele ya PAC Jumanne jioni, kukataa kutaja jina la Bi Kariuki kama Waziri aliyetumia huduma za helikopta.

Hata hivyo, wanachama wa kamati hiyo walimlazimisha Katibu Kimonye kukubali kuwa Bi Kariuki ndiye alikuwa Waziri wa Utumishi wa Umma na Masuala ya Vijana wakati huo.

“Kumbuka kwamba ukiendelea kumkinga, wewe ndiye utaelekezewa lawama hiyo,” Bw Wandayi akamwonya huku akiungwa mkono na Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale. Bw Duale pia alimtaka Bi Kimonye kufichua jina la Waziri aliyeabiri helikopta hiyo na mmiliki wake.

“Hauwezi ukaficha maelezo. Tukitaka kumtambua huyo mtu tutaweza; kile tutafanya ni kupiga simu kwa mamlaka ya kusimamia safari za angani na maelezo. Tunaweza pia kupata habari kutoka kuwa afisa wa kitengo cha ujasusi ambaye alikuwepo wakati Waziri huyo aliabiri ndege hiyo,” akasema Bw Duale.

Mbunge wa Funyula Wilberforce Oundo pia alimshutumu Bw Kimonye kwa kudinda kufichua jina la Waziri aliyeabiri helikopta hiyo.

You can share this post!

NLC yataka maskwota wa tangu ukoloni sasa wapewe makao

Matiang’i aahidi kuanika walanguzi wa mihadarati