MAUYA OMAUYA: Nyachae alikuwa na bidii, ila alikuwa ‘mkoloni mweusi’

Na MAUYA OMAUYA

KANDO na bidii yake binafsi, ni bayana kwamba ufanisi wa Simeon Nyachae ni zao la maovu ya ukoloni.

Wanyama wote sio sawa. Katika hotuba moja, El Shabaaz Malcolm X , mpiganiaji wa haki za raia weusi nchini Amerika alifafanua kwamba hata wakati ule mgumu wa majonzi na vilio vya utumwa, watumwa walikuwa sampuli mbili. Kulikuwepo na watumwa wa ndani, na watumwa wa nje kwenye mashamba ya utumwa.

Mtumwa wa ndani aliishi kwa karibu sana na yule bosi bahili. Mienendo yao ilifanana. Mtumwa wa ndani alikula kile alichokula bosi, alivaa jinsi bosi alivaa na kwa kila jambo alikubaliana na katili yule.

Bosi alimwamini kijakazi huyu wa ndani. Katika fikira zake na ndoto zake, huyu mtumwa alijiona sawa na bosi katika mambo yote na alihusudu cheo na mamlaka ya kachinja huyu.

Malcolm X anasema mtumwa wa ndani alimjali na kumpenda bosi hata kuliko bosi alivyojipenda mwenyewe. Bosi akiugua, mtumwa wa ndani alihisi maumivu katika moyo na nafsi yake.

Mtumwa huyu hakuona hata haja ya kujinasua kutoka kwa minyororo ya utumwa kwa sababu mawazo yake hayakuwa na upana kuthamini maisha mbali na bosi.

Alikuwa kibaraka na alitumiwa na bosi kudhulumu na kukandamiza watumwa wengine.Halafu kulikuwepo watumwa wa nje. Idadi yao ilikuwa kubwa na walibeba mateso yote ya utumwa. Waliishi kwa dhiki na uhaba mabandani, mavazi yao raruraru yamechanikachanika, miili imedhoofika kwa njaa, kichapo na uchofu.

Walipopata mlo, ilikuwa makombo na mabaki tu.Katika kila hatua walipigana kujikomboa na kujitwalia uhuru, haki na usawa kwao na kwa vizazi vyao.Hali hii imejirudia wakati wa ukoloni humu nchini na kote barani. Waliopigana jino na ukucha kujitawala na kurejesha uhuru wa mataifa yetu ni wa kitengo cha pili.

Wakati huo huo, kulikuwepo ‘wakoloni weusi’ ambao kwa kila njia walitumiwa kutekeleza hila za wakoloni. Nchini Kenya hasa, wakoloni walitumia viongozi hawa kama vibaraka kuhalalisha au kulazimisha unyakuzi wa ardhi, mali ya wenyeji na jasho la Waafrika.

Wakati wa vita vya kujikomboa wengi wa ‘watumwa hawa wa ndani’ walikuwa wasaliti dhidi ya makundi kama Mau Mau. Kama zawadi kwa huduma za usaliti wengi walituzwa elimu na mali na kuwekwa kileleni mwa daraja za jamii zao.

Ni katika ligi hiyo ya ukoo ambako Simeon Nyachae alizaliwa kwa chifu wa kikoloni Musa Nyandusi. Kuna majina mengine tajika kama chifu Njonjo, chifu Koinange, chifu Tengecha, mfalme Mumia na wengine kadha kote nchini.

Machifu hawa walijifunza mbinu za utapeli wa kikoloni na wakazitia makali maradufu. Waliwatumia Waafrika wenzao kama watumwa, walitwaa kodi haramu kujinufaisha, walinyakua mashamba na mifugo na kwa kila jambo wao na jamaa zao waliishi kama wakoloni kutoka Uingereza.

Yamkini, kila uozo tuliopokezwa baada ya uhuru ulitekelezwa na kuendelezwa kupitia kwa hawa ‘wakoloni weusi’.Katika nchi ambako wenyeji walikuwa wanaozeana katika dhuluma, jamaa za machifu hawa waliishi katika starehe na fahari. Hatimaye jamaa hawa hawa walirithi nafasi za kutajika kwenye utawala wa nchi mnamo mwaka wa 1963 Kenya ilipojinyakulia uhuru.

Huku taifa changa likijitahidi kupambana na umaskini, ujinga na maradhi hayo kwao ilikuwa hekaya tu, walikuwa wakwasi walonavyo tayari. Kila jitihada walizofanya maishani walikuwa na msukumo na viwezesho kutoka kwa historia zao. Walikuwa na elimu, mali na uzoefu wa kutawala.

Dkt Mbiyu Koinange kwa mfano alikuwa mkenya wa kwanza kuhitimu shahada ya PhD. Shina lake ni Chifu Koinange wa kikoloni. Vivyo hivyo ufanisi wa Nyachae umeota kutoka shina la chifu Nyandusi wa kikoloni.

Ikiwa kwa mfano, tutabadili jina la uwanja michezo wa Kisii kuwa la ‘Simeon Nyachae’ kama kielelezo cha bidii na ushujaa wake, tutakuwa tunasaliti ukweli na historia ya jamii na taifa.

Tutasalia na kovu moyoni hasa ikizingatiwa kuwa wengi wa jamaa za mashujaa halisi wa uhuru wametupwa katika kaburi la sahau.

mauyaomauya@live.com