• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 4:25 PM
Wanajeshi wakataa kupokea chanjo ya corona

Wanajeshi wakataa kupokea chanjo ya corona

NA AFP

WASHINGTON, AMERIKA

IDADI kubwa ya wanajeshi wamekataa kupokea chanjo ya virusi vya corona licha ya maambukizi kuongezeka katika idara hiyo.

Maafisa wa makao makuu ya jeshi la Amerika, jana walifichua kwamba theluthi moja ya wanajeshi wamekataa chanjo inayoendelea kutolewa.

Meja Jenerali Jeff Taliaferro, alifichua kwamba wanajeshi hawajakumbatia chanjo hiyo ambayo idara hiyo imetaja inatolewa kwa hiari. Hii ni kwa sababu kitengo kinachoidhinisha chanjo na matumizi ya dawa hakijatoa idhini ya chanjo hiyo kutolewa kwa lazima katika idara ya jeshi na kwa raia.

“Ni theluthi mbili pekee ambao wamepokea chanjo hiyo. Idadi hiyo haijajumuisha data ya jeshi zima,” akasema Taliaferro. Msemaji wa jeshi la Amerika, John Kirby, naye alisema kuwa zaidi ya wanajeshi 916,000 wamepokea chanjo hiyo na akasisitiza kuwa wanaokataa wanafanya hivyo kutokana na hofu ambayo pia raia wako nayo kuhusu ufanisi wa chanjo hiyo.

Serikali ya Rais Joe Biden inaonekana imekuwa ikiwatumia wanajeshi wakumbatie chanjo hiyo kisha kuwashawishi raia kuwa ni salama kwao.

Kirby alifafanua kuwa kufikia mwisho wa wiki hii, zaidi ya wanajeshi milioni moja watakuwa wamepewa chanjo hiyo dhidi ya virusi vya corona.

“Kwa sasa sheria haituruhusu kumlazimisha kila mwanajeshi kupata chanjo pamoja na familia zao,” akasema Kirby. Alifichua kuwa Waziri wa Ulinzi, Lloyd Austin, ameongoza kwa kuwa mfano na tayari amepokea chanjo hiyo.

“Kile ambacho waziri anahitaji ni kuhakikisha kila mwanajeshi anajiamulia bila kulazimishwa. Msukumo huo unatokana na kujali afya zao na za familia zao,” akaongeza.Kwingineko, watu wazima wanaoishi katika mji wa Serrana, Brazil jana walianza kupokea chanjo ya corona.

Brazil ni nchi ya kwanza kutoa chanjo hiyo kwa watu wengi ikilenga kudhibiti maambukizi yanayozidi kupanda nchini humo.Chanjo hiyo inalenga watu 30,000 kati ya 50,000 wanaoishi mjini humo.

Pia itawasaidia wanasayansi kubaini ufanisi wake huku maambukizi ya corona yakichipuka tena Brazil yenye zaidi ya watu milioni 212.Hata hivyo, wanawake wajawazito na wanaonyonyesha na raia wanaougua maradhi mengine ndio hawatapata chanjo hiyo katika mji huo ambao ni wa umbali wa kilomita 300 kutoka Sao Paulo.

“Tumekuwa tukisubiri chanjo hii sana. Nina matumaini itatulinda dhidi ya corona,” akasema Edson Jose Felix, 81 akiwa na mkewe Margarida, 80.Zaidi ya wahudumu wa kiafya 500 ndio watatoa chanjo hiyo ambayo dozi 60,000 itatumika kisha ufanisi wake utathminiwe baada ya mwaka moja na nusu.

You can share this post!

Kisiwa cha matajiri ‘kuwafuga’ maskini

WANDERI KAMAU: Tujinasue sasa kutoka kwa mfumo wa kibepari