• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
MWANAUME KAMILI: Haiwezekani kushiriki uovu ukaepuka dosari!

MWANAUME KAMILI: Haiwezekani kushiriki uovu ukaepuka dosari!

NA OBENE AMUKU

Hatuna budi kuchukua hatua zifaazo kubadili maisha yetu hasa akina sisi tunaolalamika juu ya wengine. Nakumbuka vyema udogoni nilipokuwa naonywa vikali juu ya tabia zangu na wenzangu tuliokwepa nyumbani na kwenda kucheza densi katika maeneo ya watu wazima.

Kweli, tulipenda sana kujificha uani ama nyuma ya kuta na kusakata ngoma kiasi cha kutiririsha jasho. Japo tulicheza tu jinsi watoto wanavyopenda vya dezo lakini wazazi, hasa mamangu alikuwa na mtazamo tofauti.

Kwa maoni yake, nilikuwa naatika mbegu mbaya mno katika shamba lenye rutuba: shamba la uhuni, anasa na utepetevu. Isitoshe, wengi wa watoto tuliocheza nao walikuwa tayari wamekwisha agana na masomo wangali mbichi.

Ndio kwanza kama mikoko, walialika maua. Yaani, waliona heri maisha ya kuzurura mitaani, kusaka matonge majalalani, kuchuuzia watu barafu na njugu! Waliona fahari mtoto kufungia sarafu zake na kuzibeba upindoni pamoja na chawa waliomo. Usingekosa angalau chawa mmoja kwenye pindo za bukta ama kanzu tulizovalia.

Ndivyo hivyo maisha yalivyokuwa. Usijehadaika kwamba kila king’aacho kilitoka kiwandani. Wengine wetu ilibidi wafinyanzi kutukazia kamba, kutuponda mfano wa vigae na mwishowe kutuchuja kabla mambo kuharibika. Ndivyo wanavyofanya wazazi wanaojua maana ya mtu kuwa mzazi.

Tatizo kubwa linalotusibu kama jamii ni kuwepo wanawake kwa wanaume wanaoishi kama uyoga. Wa kwenda Ijumaa kujivinjari vilabuni wakarudi Jumamosi asubuhi wakiwa wameoa ama wameolewa.Wanaondoka kwenda sokoni kutafuta vya sokoni lakini wanapofika huko, wanakuwa ndio soko la watu.

Viko wapi vigezo na hadhi ya mwanamke na mwanamume kamili? Afadhali maembe ya jioni, angalau bei yao nafuu. Akina sisi tunakwenda tu kwa kufuata upepo na pepo zake.

Tumeshuka bei na thamani yetu iko nyayoni. Ndio maana tunajikuta tumeoa ama tumeolewa wa watu tusiojua hata majina yao. Ndio maana tunasononeka kila kukicha maana tuliolewa na kuoa watu wasioweza hata kutushauri kwa jambo.Wangapi kati yenu watu wazima mnatenga hata muda wa mazungumzo ya kifamilia?

Yaani mke na mumewe wakaketi zuliani wakazungumzia ya muhimu, wakapigana mabusu wakiwa papo hapo zuliani? Maisha ya leo yanahitaji uhuru! Wangapi kati yenu mnaweza kumtuma mume ama mke kwenye akaunti zenu binafsi?

Kuna wanaume wanafanya kazi lakini wake zao hawajui hata mshahara wanaopokea kila mwezi. Wanaume ndio kwanza wako pabaya. Wanaishi na kuzalisha wanawake lakini hawana habari juu ya jambo lolote katika maisha ya mwanamtu!

Hizo ndizo tunazoita ndoa za karne hii. Mabozi hawa wanakutana tu usiku, tena gizani kwa shughuli za giza na kila mmoja akaangukia kwake hadi asubuhi.Nasikitikia sampuli ya watu wazima wanaofanya mambo bila tafakuri.

Hawajui maana ya mtu kutumia vigezo vya maisha na kuratibu mipango na hali kwa mujibu wa vigezo hivyo. Kama wewe ni mwanamke, bila shaka umewahi kutana na dume na cha kwanza kilichofika akilini mwake ni “urembo wa nyonga zako” ama “ubora na dodoki zako!”

Yaani mwanamume anakusifia vya ndani ilhali hajui jina wala kondeni kwenu. Labda hamjui nyonga ni sehemu gani mwilini.Wanawake wanakisiwa kuwa na maumbo ya kupendeza nyongani.

Sijui nani amekwisha kufika huko akasaza nyonga za majike. Haidhuru! Nyonga ni kati ya kiuno na goti. Sasa tafakari akili za mwanamume anayekuwazia nyongani kabla hata kukujua jina.

Tulivyo majike machizi yasiyojua te wala be, tunasisimkia mno hao wanaopenda nyonga zetu kuliko wanaume wanaotusukuma kwenda shule tukapevuke akili kabla kutia mikono kwenye ratili “kupima uzito wa mume!”

Ndio nyinyi watoto wa watu mnaotaka kuolewa na mwanamume kwa kuwa ameweka funguo za gari mezani. Mbona basi msikwende mkaolewa na maduka yaliyoegeza magari?

Vipi mwanamtu utaolewa eti kwa sababu “mume ana gari nzuri?” Je, wewe una nini unacholeta ili kwa pamoja mkajenge familia thabiti? Tumefanya mazoea kutafuta waliofika ilhali sisi wenyewe hatujaanza hata safari. Maisha ni kushikana mikono, kushikamana, kufaana kabla kufanana kihali!Kama nilivyosema juu ya maisha udogoni.

Sijui ningalikuwa nini kama ningaliachwa kucheza densi, kuchuuza njugu na barafu, kula majalalani na kukwepa masomo. Nasema sijui ningekuwa nini maana wote tulioshirikiana udogoni hawako tena wala siwezi kuona walichoafikia wakatimiza maishani. Walipotea ama niseme walipotelea kuko huko wanakopotelea watu waliochagua maisha ya utepetevu.

Wengine walipotezwa baada ya kushindana na mkono mrefu wa sheria. Wengine walidondoka juu ya matwana walipokuwa wanasaka riziki kama utingo, maisha ikawatinga na kuwatokomeza.

Funzo la muhimu ni kwamba mtu huchagua mwenyewe kukaa nyumba mfano wa mkia. Haiwezekani kushiriki uovu mwanamume ama mwanamke ukaepuka dosari na shinikizo za kuiga vitendo hivyo duni. Chukua hatua kubadili mkondo wa maisha. Hivyo ndivyo anavyofanya mwanamume na mwanamke kamili.

[email protected]

You can share this post!

Elachi atunukiwa Unaibu Waziri Uhuru akipanua serikali yake

FATAKI: Imarisha chombo chako uweze kupiga mbizi baharini...