• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
Utata wa uteuzi wa Mwende Mwinzi waendelea kutokota

Utata wa uteuzi wa Mwende Mwinzi waendelea kutokota

DAVID MWERE na CHARLES WASONGA

MAKABILIANO yananukia kati ya wabunge na serikali kuu kufuatia kuidhinishwa na uteuzi wa Mwende Mwinzi kuwa balozi wa Kenya nchini Korea Kusini.

Wabunge sasa wnalalamika kuwa uteuzi wa Bi Mwende unaenda kinyume na uamuzi wao wa 2019 wa kukataa uteuzi huo hadi suala la urais wake wa mataifa mawili lisuluhishwe.

Wakiongozwa na Mbunge wa Masop Vincent Tuwei wabunge walisema uidhinishwaji wa uteuzi huo ni haramu, ikiwa ni kweli ulifanyika kabla ya Bi Mwende kuasi uraia wake wa Amerika.

Wakati wa kuhojiwa kwake kwa wadhifa huo Bi Mwende aliungama kuwa ana uraia wa Kenya na Amerika. Alizaliwa Amerika na baba Mkenya na mama Mwamerika.

Hata hivyo, alipoelezwa kuwa ni kinyume cha sheria kwa mtu mwenye urais wa nchi mbili kuteuliwa kwa wadhifa mkuu kama wa balozi, Bi Mwende alikataa kuasi uraia wake wa Amerika.

Hii ndio maana Kamati ya Bunge kuhusu Ulinzi na Mashauri ya Kigeni, katika ripoti yake iliwasilishwa bungeni, Septemba 29, 2019 ilidinda kuidhinisha uteuzi wake.

Kwenye mapendekezo yake, yaliyoidhinishwa na kikao cha bunge lote, kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Kajiado Kusini Katoo Ole Metito, ilisema sharti suala hilo la uraia wa nchini mbili utatuliwe kwanza kabla ya Bi Mwende kupewa idhini ya kuhudumu kama Balozi wa Kenya nchini Korea Kusini.

Lakini mnamo Februari 17, Jumatano, picha zilipeperusha kwenye runinga za humu nchini zikionyesha Bi Mwende akawasilisha stakabadhi zake kwa mamlaka ya Korea Kusini, ishara ya kukubalika kwa balozi wa Kenya.

Mnamo Februari 18 Bw Tuwei alimtaka kiongozi wa wengi Amos Kimunya kuthibitisha ikiwa Bw Mwende alitumwa jijini Seoul baada ya kuasi uraia wake wa Amerika au la.

“Kiongozi wa wengi anafaa kuthibitisha ikiwa ni kweli Bi Mwende aliteuliwa rasmi na akaripoti nchini Korea Kusini. Pia anafaa kuthibitisha ikiwa aliasi uraia wake wa Amerika kabla ya uteuzi huo kufanywa, au la,” akasema.

Wabunge wametisha kuinyima fedha ubalozi wa Kenya nchini Korea Kusini, katika mwaka wa kifedha wa 2021/2022 ikiwa Serikali Kuu ilikaidi bunge la kuteua Mwende kabla yake kuasi urais wa Amerika.

You can share this post!

FUNGUKA: Msisimko wangu wa mahaba hutokana na kutazama...

BBI: Magari kwa madiwani, wilbaro kwa vijana