• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Ugonjwa usiojulikana wafyeka kondoo 2,000 Gilgil

Ugonjwa usiojulikana wafyeka kondoo 2,000 Gilgil

Na SAMMY WAWERU

WAFUGAJI Kaunti Ndogo ya Gilgil wanaendelea kukadiria hasara ya kupoteza kondoo kutokana na mkurupuko wa ugonjwa usiojulikana.

Wanasema maradhi hayo ambayo dalili zake ni kondoo kuendesha na kupoteza uzani, yameangamiza zaidi ya kondoo 2, 000. Kulingana na mfugaji Stephen Sururu, ugonjwa huo ulilipuka mwaka uliopita, 2020.

“Tumepoteza zaidi ya kondoo 2, 000. Haueleweki, wanapoathirika wanaendesha na kupoteza uzani na chini ya mwezi mmoja wanafariki,” Mzee Sururu akaambia Taifa Leo Dijitali kwenye mahojiano ya kipekee, katika eneo la Nagum, Kaunti Ndogo ya Gilgil.

Mbali na Nagum, maeneo mengine yaliyohangaishwa na ugonjwa huo ni pamoja na Nyama Choma, Oljorai na Eburu.

“Licha ya kujaribu kutegua kitendawili, hatujapata suluhu. Tunaendelea kukadiria hasara mifugo wetu wakiangamia,” akasema mfugaji mwingine.

Kando na kondoo, ugonjwa huo pia unaathiri mbuzi, ila kwa mujibu wa wafugaji tuliozungumza nao kondoo ndio wamewezwa.

Mzee Sururu, 68, alisema amekuwa mfugaji tangu utotoni mwake na kwamba hajawahi kushuhudia maradhi yenye athari za aina hiyo kwenye mifugo.

Alisema wafugaji wanapania kupeleka baadhi ya kondoo na mbuzi walioathirika katika maabara ya ukaguzi wa mifugo, ila ubovu wa barabara unawatatiza kuwasafirisha.

“Miundomsingi kama vile barabara eneo hili ni mbovu zaidi. Kupeleka mifugo waliougua ni kibarua,” mfugaji huyo akalalamika.

Licha ya wakazi maeneo yaliyoathirika kuwasilisha kilio chao kwa viongozi waliochaguliwa, wanadai hakuna yeyote aliyewapa majibu kutafutia mifugo wao tiba.

Isitoshe, wanahoji viongozi wameendelea kufumbia macho hali mbaya ya miundomsingi.

You can share this post!

Kufungwa kwa hoteli ya kihistoria pigo kwa maskauti

Fujo tena katika mikutano ya Ruto na Raila