Fujo tena katika mikutano ya Ruto na Raila

Na CHARLES WASONGA

POLISI Jumamosi katika kaunti za Homa Bay na Baringo waliingilia kati kuwakabili vijana waliojaribu kuvuruga hafla zilizohudhuriwa na kiongozi wa ODM Raila Odinga na Naibu Rais William Ruto.

Katika hafla ya mazishi iliyohudhuriwa na Bw Odinga katika Shule ya Upili ya Ratanga eneobunge la Ndhiwa, kaunti ya Homa Bay makundi mawili ya vijana yalirushiana Makonde mbele ya kiongozi huyo.

Iliwalazimu polisi kuingilia kati na kuwacharaza kwa marungu na mijeledi kuwaondoa karibu na hema ambako Bw Odinga alikuwa ameketi.

“Vijana mtulie. Mnyamaze. Tumkaribishe baba kwa njia ya heshima. Vijana tafadhali mkomeshe fujo. Sote tutulie,” mratibu wa shughuli hiyo alisikika akisema.

Hata hivyo, chanzo cha makabiliano baina ya vijana hao hakikubainika. Katika mji wa Kabarnet, kaunti ya Baringo, Dkt Ruto pia alikumbana na kundi la vijana ambao walijaribu kuvuruga mkutano wake wa hadhara.

Hata hivyo, Naibu Rais aliwaomba wafuasi wake kumsikiza na wawapuuze vijana hao.

“Ningependa kuwaambia wale ambao wanawahonga vijana kwa kuwapa pesa kwamba hawatafaulu. Vijana wa Kabarnet wameelimika na wako na akili.

“Wale ambao wanataka kuchochea fujo watumie wake na watoto wao badala ya kuwatumia watoto wa wengine,” Dkt Ruto akasema.

Katika kaunti ya Nakuru, polisi walitumia vitoa machozi kutawanya mkutano wa kampeni katika wadi ya London, uliopangiwa kuhutubiwa na wandani wa Dkt Ruto; Susan Kihika (Seneta wa Nakuru) na wabunge Kimani Ngunjiri (Bahati) na Mohammed Ali (Nyali).

Polisi walikabiliana na wafuasi wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) ambao wamefika eneo hilo kwa kampeni ya kumpigia debe mgombea wa chama hicho Nzuki Wachira.

Maafisa hao wa usalama ambao walitumia vitoa machozi kuwatawanya raia kabla ya kuliziba uwanja ambapo viongozi hao walipangiwa kuhutubu.

Habari zinazohusiana na hii

KONDOO WA RUTO MATAANI

UHURU AMTULIZA RAILA