• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:30 PM
HARRIET KWAMBOKA: Ipo siku nitatesa katika tasnia ya uigizaji

HARRIET KWAMBOKA: Ipo siku nitatesa katika tasnia ya uigizaji

Na JOHN KIMWERE

UKWELI wa mambo ni kwamba wahenga waliposema penye nia pana njia hawakupaka mafuta kwenye mgongo wa chupa, maana ndivyo ilivyo tangu zama hizo mpaka sasa.

Usemi huo umeonyesha mashiko ya haja miongoni mwa jamii. Aidha ni msemo unaozidi kudhihirishwa na wengi ambao wameamua kujituma kisabuni kwa kujiamini wanaweza huku wakipania kutimiza maazimio yao maishani.

Harriet Kwamboka Charles anaamini anacho kipaji cha kufanya vizuri katika masuala ya uigizaji anakolenga kuibuka staa wa kuigwa na wengi hapa nchini.

“Ingawa sijapata mashiko katika tasnia ya uigizaji ninatamani sana kutinga upeo wa kimataifa miaka ijayo. Ni jambo ninalolizamia kwa udi na uvumba.” Kisura huyu aliyeanza kujituma katika masuala ya maigizo mwaka 2018 anadokeza kuwa ipo siku kazi zake zitakumbalika.

”Bila kujipigia debe ninaamini ninatosha mboga kufanya vizuri katika uigizaji endapo nitapata nafasi na mwelekeo mzuri. Katika mpango mzima natamani sana kushiriki filamu na zipate mpenyo kupeperushwa kwenye runinga ili kunijenga taaluma,” akasema.

Dada huyu hufanya kazi na kundi la Thee Alpha Arts production ambalo huzaliwa filamu kupitia mwogozo wa vitabu za riwaya (Set Books). Kabla ya kujiunga na kundi hilo anajivunia kufanya kazi na kundi la Grand Artways production awali likifahamika kama Grand Artspan Production.

Dada huyu anajivunia kushiriki filamu iitwayo ‘Vituko mitaani’ ambayo huoneshwa kupitia runinga ya mtandaoni inayokwenda kwa jina Hollywave TV.

Pia ameshiriki kipindi cha kuvunja mbavu cha Kababa Comedy. Kipusa huyu anasema kuwa katika uigizaji analenga kufikia hadhi ya msanii wa Kenya, Lupita Nyong’o anayetamba katika filamu za Hollywood. Kadhalika anadokeza kuwa ana kiu cha kumiliki brandi ya kuzalisha filamu ili kukuza talanta za wasanii chipukizi nchini.

Msichana huyu aliyezaliwa mwaka 1999 anasema akiwa mtoto alitamani sana kuhitimu kuwa mwana habari lakini maisha yalimwendea mrama.

Kwa waigizaji wa humu nchini dada huyu anasema angependa kufanya kazi na wasanii kama Yasmeen Saedi (Maria) mhusika mkuu kwenye kipindi cha Maria ambacho hupeperushwa kupitia runinga ya Citizen TV.

Pia anasema anatamani kujikuta jukwaa moja na Cate The Actress. Kwa wasanii wa filamu za Kinigeria (Nollywood) anasema angependa kupiga shughuli nao Destiny Etieko na Mercy Johnson.

Anashauri wenzie kuwa makini kwa kile wanachohitaji wanapojiunga na sekta ya uigizaji. ”Kama ilivyo kwa sekta zingine jukwaa la maigizo kamwe mambo sio mteremko limejaa pandashuka nyingi tu ambapo ni rahisi kwa msanii kupoteza mwelekeo endapo atasahau azma yake,” akasema.

Aidha anasema kwamba uigizaji unahitaji kuvumilia maana mafanikio hayapatikani rahisi. Anadokeza kuwa ingekuwa vizuri kama serikali inaweza kutega fedha za kusaidia sekta ya uigizaji maana wapo wasanii wengi tu humu nchini ambao hawajapata nafasi kuonyesha vipaji.

You can share this post!

KENNEDY WAMBUA: Tambua mtindo mpya wa usanii...

THOMAS OLYBOLE: Kenya ina uwezo wa kuandaa filamu za...