• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
RAEL ODIPO: Uigizaji si mzaha, lazima ujitume

RAEL ODIPO: Uigizaji si mzaha, lazima ujitume

Na JOHN KIMWERE

NI ndoto ya kila msanii kuona anaimarika katika sanaa yake na kutambulika kote duniani. Rael Adhiambo Odipo ni kati ya kina dada ambao hawataki kuachwa nyuma wanaopania kujizolea umaarufu sio haba hapa nchini pia kimataifa akilenga kuibuka miongoni mwa wasanii tajika kama mwigizaji pia mwanamuziki wa nyimbo za injili.

Kando na hayo dada huyu aliyezaliwa mwaka 1995 ni mpodoaji (Makeup Artist) bila kusahau kuwa huwavalisha wasanii na watu wengine wakati wa hafla mbali mbali.

Msichana huyu anasema bila kujipigia debe anaamini anacho kipaji cha kutesa katika jukwaa la filamu na kufanya vizuri miaka ijayo. Katika mpango mzima kisura huyu anasisitiza kuwa anatamani sana kujituma katika masuala ya maigizo na kufikia hadhi ya mwigizaji anayezidi kutamba katika sekta ya maigizo duniani mzawa wa Kenya, Lupita Nyong’o.

Chipukizi huyu ni kati ya wanadada wengi tu wanaoendelea kuvumisha sekta ya uigizaji hapa nchini. ”Natamani sana kuibuka kati ya waigizaji bora nchini pia kumilika brandi yangu ya kuzalisha filamu ili nipate fursa ya kukuza waigizaji wanaoibukia,” alisema na kuongeza kuwa ana imani tosha ipo siku atakubalika kama wenzake waliotangulia katika tasnia ya uigizaji.

Anasema kuwa alivutiwa na masuala ya maigizo baada ya kutazama filamu iitwayo ‘Smart Servant’ yake Mercy Johnson aliye miongoni mwa wasanii mahiri nchini Nigeria.

Ingawa kichuna huyu alianza kujituma katika masuala ya maigizo miaka mitano iliyopita anajivunia kushiriki filamu chache ambazo tayari zimepata mpenyo na kuonyeshwa kwenye runinga tofauti hapa nchini. Kwa maigizo dada huyu ameshiriki ‘Maisha bure (ilioneshwa QTV),’ ‘Kenyan Movie (ilioneshwa K24)’ na ‘Hulabaloo (ilioneshwa Maisha Magic East).’

Tangia aanze uimbaji anajivunia kughani fataki mbili; ‘Yesu anaweza’ na ‘Nyasaye Ber (Mungu ni Mwema)’. Hata hivyo anadokeza kuwa nyimbo nyingi zimo jikoni anatarajia kuziachia hivi karibuni.

Msichana huyu ambaye tangia akiwa mtoto alitamani kuhitimu kuwa mwanajeshi  na kufanya kazi na kikosi cha Marekani kamwe sio mchoyo wa mawaidha. Anashauri wenzie wafahamu kuwa uigizaji sio kazi rahisi pia wajitume na kujiamini kwa chochote wanachofanya.

Anasema sekta ya maigizo imejaa changamoto ikiwamo ubaguzi miongoni mwa maprodusa kwa misingi ya tabaka bila kuweka katika kaburi la sahau maumbile.

”Itakuwa vyema endapo maprodusa watakomesha mtindo wa kuwapendeleo wengine ambapo nina imani tosha kuwa wakitoa nafasi kwa waigizaji chipukizi watakuwa wanaijenga,” akasema.

Anasema kwa waigizaji wa kigeni angependa kutua jukwaa moja na waigizaji mahiri nchini Nigeria akiwamo:Mercy Johnson aliyeshiriki filamu kama ‘My choice’ na ‘International High Class Maids’ kati ya zingine. Pia Destiny Etiko aliyeigiza ‘Loving in Poverty’ na ‘Desperate Triplet.”

You can share this post!

THOMAS OLYBOLE: Kenya ina uwezo wa kuandaa filamu za...

SALOME NJERI: Mtambue ‘Mama Chapo’ wa kipindi...