• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Blue Boys yatwaa ushindi wa KYSD

Blue Boys yatwaa ushindi wa KYSD

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya wavulana ya Blue Boys kwa wasiozidi umri wa miaka kumi imejitahidi na kuibuka mabingwa wa Ligi ya Kinyago Youth Sports Development (KYSD) muhula huu wa 2020-21.

Timu hiyo ambayo hutiwa makali na kocha, Newton Sakwa ndio ilikuwa mwanzo kushiriki ligi hiyo na kufanikiwa kuibuka mabingwa kati ya vikosi 14 vilivyoshiriki kinyang’anyiro cha msimu huu. Kwenye mchezo wa mwisho kuamua nani bingwa wa kipute hicho chipukizi hao chini ya nahodha, James Bradney walisajili ufanisi wa bao 1-0 dhidi ya Young Lions lililofunikwa kimiani na Ryan Ehenzo.

Kikosi hicho kimetuzwa mabingwa wa ngarambe hiyo baada ya kumaliza ratiba ya mechi hizo kwa kufikisha pointi 33. Nayo timu ya Young Lions ilimaliza ya pili kwa kusajili alama 30, sawa na Kawanga FC pia Young Elephant tofauti ikiwa idadi ya mabao. Nayo Makongeni Youth inafunga tano bora kwa kuvuna alama 23, moja mbele ya Kinyago United.

”Kiukweli nina furaha tele kwa ufanisi wa chipukizi wangu licha ya kuwa ndio mwanzo tulioshiriki mechi za kinyang’anyiro hicho.Tayari nimegundua tunazo talanta nyingi mitaani zinazohitaji kushikwa mikono,” kocha huyo alisema na kuongeza kuwa kituo hicho kinasaidia chipukizi wengi kutoka mitaa mbali mbali. Aidha kocha huyo anasema haikuwa rahisi maana timu zote zilikuwa zimejipanga kupigania taji hilo.

Kocha huyo anadokeza kuwa wamepania kuanza mazoezi mapema kujinolea kampeni za kipute cha msimu ujao. Anakiriri kuwa ana imani endapo wataanza maandalizi yao mapema chipukizi wake watapigana mwanzo mwisho na kuhifadhi taji hilo.

MITAA MBALI MBALI

Afisa mkuu na mwanzilishi wa KYSD, Anthony Maina anasema kipute hicho huleta pamoja timu kutoka maeneo tofauti ikiwamo: Mukuru kwa Njenga, Makongeni, Kaloleni, Bahati, Madiwa, Eastleigh South ward, California, Biafra, Kinyago, Kanuku, Majengo, Shauri moyo, Mashimoni na Kaiyaba.

Kocha Newton Sakwa anatoa wito kwa wahisani wajitokeze kukipiga jeki kituo cha KYSD maana kimekuwa katika mstari wa kwanza kwenye jitihada za kunoa talanta za chipukizi wa soka katika mtaa wa Kinyago.

KIKOSI

Blue Boys inajumuisha:Ryan Ehenzo, Godfrey Chacha, Joe Ambundo, Michael Jenabi, Simson Masinde, James Bradney, Vincent Onyango na Elvis Erambo, Emmanuel Jayden. Pia wapo Wayne Munyao, Travis Njoroge, Carlos Albert, Paul Kegode, Kelvin Muindi, Jeremy Ryan, Bravin Sakwa, Philip Musyoka na Dennis Musyoka. Timu zingine zilizoshirikisha kinyang’anyiro hicho zikiwa: Sharp Boys, MASA, Young AC, Kaiyaba Young and Sports Association (KYSA), Gravo Legends, Locomotive, Fearl FC na Arizen Soccer Academy.

You can share this post!

Siri ya Young Elephant kutetemesha ligi

Familia 100 zakesha kwa baridini baada ya nyumba zao...