• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
JAMVI: Mrengo wa Weta, Musalia, Kalonzo, Moi watia Raila, Ruto wasiwasi

JAMVI: Mrengo wa Weta, Musalia, Kalonzo, Moi watia Raila, Ruto wasiwasi

Na CHARLES WASONGA

HATUA ya viongozi wa vyama vya Wiper, KANU, Amani National Congress (ANC) na Ford Kenya kudokeza kuwa muungano wao utateua mgombea mmoja wa urais 2022 unaonekana kuwaingiza baridi Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Hii ndio maana Dkt Ruto sasa ametaja vuguvugu hilo maarufu kama “One Kenya Movement”(Vuguvugu la Kenya Moja) kama muungano wa kikabila ambao umuhimu wake umepitwa na wakati.

Kwa upande wake, Bw Odinga anaonekana kuendelea na mpango wake wa kusuka muungano mpya baada ya kuonekana kutorokwa na washirika wake katika NASA, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula. Watatu hao wamemnasa mshirika mpya, mwenyekiti wa Kanu, na Seneta wa Baringo Gideon Moi.

Hii ndio maana ameonekana kuanza kubuni muungano mwingine utakaoshirikisha wagombeaji urais wengine kama vile Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Maendeleo (UNCTAD) Mukhisa Kituyi.

Alhamisi, Odinga alikutana na wawili hao kwa kikombe cha chai katika mkahawa mmoja Nairobi ambapo inadaiwa siasa za 2022 zilijadiliwa kwa kina.Japo, awali, Mabw Musyoka, Moi, Mudavadi na Wetang’ula walisema kuwa waliungana kwa ajili ya chaguzi ndogo za Machakos, Matungu na Kabuchai sasa wameweka bayana kwamba mshikamano wao unalenga kuhakikisha mmoja wao anaingi Ikulu mwaka ujao.

Wakiongea Jumatano katika mkutano wa hadhara wa kumpigia debe mgombeaji Ford Kenya katika kinyang’anyiro cha kiti cha ubunge cha Kabuchai, Majimbo Kalasinga, viongozi hao walisema wako tayari kuchukua uongozi baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuondoka afisini mwaka ujao.

“Safari ya kuelekea Ikulu imeanza rasmi hapa Kabuchai,” akatangaza Bw Wetang’ula akiongeza kuwa wote wanne wana sifa ya kuongoza Kenya baada ya Rais Kenya kustaafu.“Mtutizame sisi wanne. Tuna umaarufu. Tuna ujuzi wa kisiasa na hatujapakwa tope la ufisadi na hivyo tunaweza kuunda serikali,” akaongeza Seneta huyo wa Bungoma.

Kauli yake iliungwa mkono na Mudavadi, Musyoka na Moi ambao walisema taifa hili halipaswi kuachwa mikononi mwa viongozi ambao wamehusishwa na sakata za ufisadi.

Huku wakimtaka Bw Odinga kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho, viongozi hao walisema wako tayari kuunga mkono mmoja wao kuhakikisha kuwa muungano unaibuka mshindi wa urais.

Wanne hao wanapania kutumia chaguzi hizo ndogo za Machakos, Matungu na Kabuchai kupima iwapo wanaweza kuzima Dkt Ruto na Odinga kisiasa. ODM kimedhamini mbunge wa zamani David Were katika Matungu huku chama kipya cha United Democratic Alliance (UDA) chake Dkt Ruto kikidhamini Bw Alex Lanya.

Katika eneobunge la Kabuchai mpeperushaji bendera ya UDA ni Evans Kakai.Vyama vya ANC, Ford Kenya, Kanu na Wiper vinashirikiana kwa kuunga mgombeaji mmoja katika kila moja ya maeneobunge hayo. Vinampigia debe Peter Nabulindo (ANC) katika Matungu na Joseph Majimbo Kalasinga (Ford Kenya) kule Kabuchai.

Wadadisi wa kisiasa sasa wanasema muungano huo umezua tumbojoto miongoni katika kambi za Dkt Ruto na Bw Odinga kwani una uwezo wa kuvuruga hesabu zao za 2022 ikizingatiwa kuwa wao ndio wamekuwa wakisawiriwa kuwa kifua mbele katika kinyang’anyiro cha urais.

“Kufikia sasa, Dkt Ruto na Bw Odinga ndio wameonekana kuwa washindani wakuu katika mchakato wa urithi wa Rais Uhuru Kenyatta. Lakini sasa ujio wa muungano wa Kalonzo, Mudavadi na maseneta Moi na Wetangula unaonekana kama mrengo wa tatu ambao bila shaka una uwezo wa kuvuruga hesabu za wawili hao,” akasema Bw Martin Andati.

Inaaminika kuwa endapo muungano huu utasalia thabiti hata baada ya chaguzi ndogo zijazo, huenda ukavuruga mipango ya Dkt Ruto na Bw Odinga ya kumrithi Rais Kenyatta.

Kwanza, huenda wawili hao wakipoteza kura za eneo pana ambalo zamani lilijulikana kama mkoa wa Magharibi na Ukambani ambazo zina idadi kubwa ya wapigakura. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kura za urais nchini hupigwa kwa misingi ya kikabila na kimaeneo.

Kwa hivyo, vuguvugu la ‘Kenya Moja’ linaweza kutapata kura nyingi katika ngome hizi za nyota wake watatu, Mudavadi, Wetang’ula na Musyoka.

Hata hivyo, Dkt Ruto bado ana uhakika wa kuhifadhi za ngome yake ya Rift Valley kwa sababu ushawishi wa seneta Moi ni finyu ilivyodhihirika juzi aliposhindwa kuwashawishi madiwani wa Baringo kupitisha Mswada wa BBI.

Hata hivyo, kubuniwa kwa muungano wa “Kenya Moja” umevuruga mikakati ya Naibu Rais kwa sababu alitegemea zaidi eneo kubwa la Magharibi ziweze kumfaa “endapo eneo la Mlima Kenya litaamua kumsaliti dakika za mwisho.”

Hii ndio maana juzi Dkt Ruto alionya Wakenya dhidi ya kupumbazwa na miungano ya kisiasa aliyoitaja kama iliyoundwa na misingi ya kikabila bali na sera zenye manufaa kwa Wakenya wote.

Alisema kuwa miungano kama hiyo haina nafasi katika Kenya ya sasa.“Tunafaa kubuniwa mawazo ya kuleta mwamko mpya miongoni mwa watu wetu. Enzi ambapo Kenya ilikuwa ikiongozwa na viongozi wa kikabila imepita,” akasema.

Dkt Ruto alisema hayo katika makazi yake rasmi Karen, Nairobi alipokutana na zaidi ya viongozi 400 wa mashinani kutoka kaunti za Nairobi, Mombasa, Nakuru na eneo pana la NyanzaAlieleza kuwa Wakenya wanahitaji muungano wa kisiasa ambao utaimarisha viwango vya maisha ya wananchi haswa wale wa chini.

“Hii ndio maana tunabuni miungano ya watu wenye mawazo endelevu kupitia vuguvugu la hasla ambalo litahakikisha kuwa rasilimali nyingi zinagatuliwa katika maeneo ya mashinani,” akasema.

Kupitia itikadi hii, Dkt Ruto aliongeza, Kenya itapiga hatua katika nyanja ya maendeleo. “Ikiwa mawazo hayo yataendeshwa na viongozi wenye maono, yataweza kuchochea uzalishaji wa ajira, mali na nafasi zingine za kujistawisha kwa Wakenya wote,” akasema.

Kwa upande wake, Bw Odinga ametangaza kuwa chama chake cha ODM kitabu muungano na Jubilee pamoja na vyama vingine vyenye maono sawa, kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

“Utakuwa muungano mkubwa. Tutaleta pamoja vyama vingine ili uwe muungano wenye nguvu zaidi. Mto Nile umeondoka Ziwa Victoria ukielekea Bahari ya Shamu na hakuna anayeweza kuuzuia,” akasema jijini Nairobi alipokutana na wenyeviti wa Jubilee na ODM kutoka maeneobunge yote 17 ya Nairobi.

You can share this post!

Shule za bweni zipigwe marufuku – Kuppet

Gachie Soccer yasaka kushiriki soka ya Taifa Daraja la Pili