Kingi akosoa wanaong’ang’ania kusalia ODM

Na MOHAMED AHMED

GAVANA wa Kilifi Amason Kingi amewashutumu baadhi ya viongozi wa Pwani wanaosema hawatakihama chama cha ODM kwa ajili ya umoja wa Pwani.

Akizungumza mnamo Jumamosi eneo la Kilifi mjini baada ya kukutana na wawakilishi wa wadi kauntini hiyo, Bw Kingi alisema ni lazima viongozi wa Pwani waungane na kuongea kwa sauti moja.

“Ikiwa sote tutasema kuwa tumewekeza ndani ya vyama tofauti, umoja wa Pwani utapatikana vipi? Leo hii mimi nisimame niseme kwamba nimewekeza ndani ya ODM kwa hivyo siwezi ondoka. Ni lazima tuwe na sauti moja,” akasema Bw Kingi.

Alionekana kulenga wabunge wawili wa Pwani – mwakilishi wa kike wa Kwale Zuleikha Hassan na mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir – ambao walisema Pwani itasalia ndani ya ODM.

Bw Nassir alisema kuwa alisema kuwa Pwani haitotoka ODM kwa sababu viongozi wa kutoka Pwani ni baadhi ya wale ambao wamechangia kukijenga na kukipa sifa chama hicho.

“Mimi binafsi na Gavana Hassan Joho pamoja na viongozi wengine tunasema kwa ujasiri kuwa tumechangia kuunda chama hichi. Hivyo basi sisi tuko ndani ya ODM mpaka mwisho,” akasema.

Bi Hassan kwa upande wake alisema kuwa Pwani imechelewa kuhusiana na mazungumzo ya kuunda chama chake na kuwataja viongozi ambao wanataka Pwani ijitoe katika chama cha ODM wanapoteza wakati kwani chama hicho ndicho kinachowafaa Wapwani.

Hata hivyo, Bw Kingi alisema kuwa jambo ambalo wanapanga ni kuleta muungano wa kisiasa wenye asilia ya hapa Pwani.

“Alisema kuwa kuna haja ya Pwani kuwa na umoja ndipo jimbo hilo liweze kuwa na sauti moja wakati nchi inaelekea mwaka wa 2022.