• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:55 AM
Covid: Serikali yaimarisha doria mpakani

Covid: Serikali yaimarisha doria mpakani

Na ERICK MATARA

SERIKALI imeimarisha ukaguzi na doria katika mji wa mpakani wa Namanga, Kaunti ya Kajiado kufuatia ripoti za kuongezeka maradufu kwa maambukizi ya virusi vya corona katika taifa jirani la Tanzania.

Licha ya kupanda kwa maambukizi hayo, Rais John Magufuli amekataa kufunga taifa hilo lakini aliamrisha wananchi wakumbatie siku tatu za maombi ambazo zilikamilika Jumapili.

Mshirikishi wa Usalama katika eneo zima la Bonde la Ufa George Natembeya alifichua kwamba serikali hailali na imeimarisha ukaguzi ili kuzuia maambukizi ya corona kuenea hadi hapa nchini.

“Tunafuatilia kwa karibu na ukaguzi umeimarishwa mpakani Namanga. Pia tunalenga kuzuia raia kutumia njia zisizotambulika maarufu kama ‘Panya routes’ ili kuzuia maambukizi ya corona. Wahudumu mpakani pia wako ange kuwapima wageni wanaoingia Kenya kutoka Tanzania,” akasema Bw Natembeya.

Naye afisa wa cheo cha juu katika wizara ya afya ambaye hakutaka jina lake linukuliwe alisema wanaendelea kutathmini na kudhibiti hali ili virusi hivyo visienee hadi nchini.

“Tunafanya juu chini na kuhakikisha kuwa kuna usalama mpakani kwa kuwapima raia wanaoingia kutoka nchi jirani ya Tanzania. Wizara ya Afya ipo makini na haitalegea ikizingatiwa tumepiga hatua kama nchi kudhibiti maambukizi ya corona,” akasema.

Kati ya viongozi ambao wanaaminika walifariki baada ya kuugua corona ni Makamu wa Rais wa kwanza wa Zanzibar Seif Sharif Hamad na mwandani wa Rais Magufuli John Kijazi. Kufikia Ijumaa Chama cha mawakili Tanzania (TLS) kilikuwa kimewapoteza mawakili 25 kutokana na virusi vya corona na kutoa wito kwa serikali kudhibiti janga hilo.

Kwa mujibu wa Rais wa TLS Rugemeleza Nshala, wana jukumu la kikatiba kuishauri serikali kuhusu masuala ya kisheria na hawataketi kitako huku raia wakiendelea kuathiriwa na virusi vya corona.

Muungano wa Makanisa Tanzania nao ulitoa taarifa ukitaka idadi ya waumini wanaohudhuria ibada wapungue makanisani huku pia ukiwataka wanaofika wahakikishe wanaketi umbali wa mita moja unusu.

You can share this post!

Kingi akosoa wanaong’ang’ania kusalia ODM

ICC huenda ifute dhamana kwa wakili Gicheru