Ruto avamia ‘bedroom’ ya Baba

Na JUSTUS OCHIENG’

NAIBU Rais Dkt William Ruto ameimarisha juhudi zake za kusaka kura katika ngome ya Kinara wa ODM Raila Odinga ya Luo Nyanza huku akilenga kumrithi Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Baada ya kutumia mbinu kali na kupenyeza kisiasa katika ngome ya Rais Uhuru Kenyatta ya eneo la Kati, Dkt Ruto sasa anaoenekana ameelekeza chambo katika ngome za Bw Odinga ili kujiweka pazuri kuingia ikulu 2022.

Maeneo mengine ambako pia amewateka waliokuwa wandani wa Rais Kenyatta na Bw Odinga ni Magharibi, Pwani na Ukambani ambako sasa anajivunia ushirikiano na aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnstone Muthama.

Duru kutoka kambi ya Dkt Ruto ziliarifu kuwa baada ya kubuni chama cha UDA chenye alama ya wilbaro, Dkt Ruto sasa anawalenga magavana Wycliffe Oparanya wa Kakamega, Hassan Joho wa Mombasa na Okoth Obado wa Migori ili kujiweka dhabiti kisiasa.

Ili kutikisa umaarufu wa Bw Odinga eneo la Nyanza, nduguye Naibu Rais, Bw David Ruto na mkewe Carol waliendesha kampeni kali za siku tatu jijini Kisumu kuanzia Ijumaa hadi Jumapili wakikutana na makundi mbalimbali ya vijana.

Mnamo Jumamosi, Bw David alizindua rasmi vuguvugu la Hustler jijini Kisumu, wakashiriki mchango wa Harambee kwa wanabodaboda wa Nyamasaria kisha wakatembelea makao ya watoto yanayopatikana eneo la Usenge katika eneobunge la Bondo, Kaunti ya Siaya.

Jumapili, nduguye Dkt Ruto alirejea Kisumu na kutembelea makao ya watoto ya Chiga eneobunge la Kisumu Mjini Mashariki ambako pia alitoa msaada kwa watoto mayatima.

“Tunazungumza lugha ya vuguvugu la Hustler ambalo linawahusisha Wakenya wote bila kujali kabila au eneo wanakotoka. Hii ndiyo maana tuko Kisumu leo na tutaendelea kuzunguka kote nchini kuimarisha hali ya maisha ya watu wetu,” akasema Bw David.

“Tunasikia baadhi ya watu wanasema kwamba baadhi ya maeneo ni ngome zao. Hata hivyo, tutafika kila eneo kwa kuwa Wakenya pia ni werevu na wanafahamu viongozi ambao wanajali maslahi yao,” akaongeza.

Mnamo 2019, mwana wa kiume wa Naibu Rais, Dkt Nick Ruto alitembelea eneobunge la Rarieda na kuongoza michango katika kanisa katoliki la Nyamasore.

Aliyekuwa kiongozi wa vijana wa Jubilee eneo la Nyanza Victor Ayugi ambaye kwa sasa ndiye anavumisha chama kipya cha UDA Jumapili alieleza Taifa Leo kwamba chama hicho kitafungua afisi zake eneo zima la Nyanza na kuvumisha urais wa Dkt Ruto.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa ODM John Mbadi na Mwekahazina Timothy Bosire wanadai kwamba Urais wa Dkt Ruto hauna nafasi yoyote katika eneo la Nyanza.

“Kama mtu anataka kuona jinsi jiji la Kisumu linavyong’aa kupitia ujenzi wa bandari na uga wa kisasa pamoja na usafi, basi yuko huru kufanya hivyo. Tunasubiri kuona iwapo atapata kura zozote,” akasema Bw Mbadi.

Bw Bosire naye alisema Naibu Rais yuko huru kutembelea eneo lolote kujiuza kisiasa ila akasema hawezi kupata uungwaji mkono wowote eneo la Nyanza.

Habari zinazohusiana na hii

Uhuru aomba talaka

Watermelon mpya?

BBI: Ruto atapatapa

Mambo yaenda segemnege