• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
Afueni kwa familia mahindi kushuka bei

Afueni kwa familia mahindi kushuka bei

Na BARNABAS BII

HUKU wakulima wakiendelea kuumia kutokana na bei duni ya mahindi Kaskazini mwa Bonde la Ufa, raia na wafanyabiashara wadogo wanaendelea kunufaika kutokana na kujaa kwa mazao hayo sokoni.

Mahindi kutoka nchi jirani za Uganda na Tanzania yamejaa sokoni huku raia wakikosa kununua pakiti ya unga madukani na badala yake kununua mahindi kisha kupeleka kwa mtambo wa kusaga kwa kuwa ni gharama nafuu.

Kampuni za kusaga mahindi nazo zinaendelea kupata hasara na zimeonya kwamba bei ya kila gunia la mahindi itaendelea kushuka zaidi huku zikitishia kupunguza idadi ya wafanyakazi wao. Kwa sasa gunia la mahindi la kilo 90 linauzwa kwa Sh2,400 kutoka Sh2,800.

Wengi wa wakulima wanaharakisha kuyauza mahindi yao huku wakijiandaa kwa msimu wa upanzi ambao unanukia mwezi ujao.

“Mahindi mengine yanatarajiwa katika masoko ya hapa nchini kutokana na muafaka wa kibiashara wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hii ni hasara kwa wakulima ambao wananunua pembejeo za kilimo kwa bei ya juu,” akasema mkulima John Too kutoka Moi’s Bridge kutoka Kaunti ya Uasin Gishu.

“Mahindi kutoka Uganda yanaendelea kuingizwa katika ukanda wa Kaskazini mwa Bonde la Ufa kupitia mpaka wa Suam. Eneo hilo ndilo ghala la chakula katika taifa zima lakini mahindi hayo kutoka nchi za nje sasa yamejaa katika Kaunti za Trans Nzoia na Uasin Gishu,” akaongeza.

Bei ya kila gunia la kilo 90 la mahindi lilikuwa limepanda hadi Sh3,000 wakati ambapo kampuni za kusaga mahindi na Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) zilikuwa ziking’ang’ania mahindi kutokana na hofu ya kupungua kwake sokoni. Hofu hiyo ilichangiwa na mavuno duni msimu uliopita.

NCPB ilikuwa ikinunua kila gunia la kilo 90 kwa Sh2,700 kutoka kwa bei ya awali ya Sh2,500 huku ikikabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa kampuni za kusaga mahindi ambazo zilikuwa zikinunua kwa Sh3,000 kutoka Sh2,700.

Hata hivyo, familia nyingi sasa zinaweza kumudu bei ya unga kutokana na kujaa kwa mahindi sokoni na wengi huhiari kujinunulia kisha kuyasaga kwa kuwa ni nafuu kuliko kununua madukani.

“Nanunua kilo mbili za mahindi kwa Sh50 kisha nasaga kwa Sh10 badala ya kununua madukani ambako unga unauzwa kwa Sh98,” akasema Rhoda Cheptoo mkazi wa eneo la Ainet, Uasin Gishu.

Kilo mbili za paketi ya unga aina ya Jimbi ni Sh98, Soko Sh100 na Jogoo Sh101 katika maduka mengi ya jumla Kaskazini mwa Bonde la Ufa.

Bei ya mbolea ya kilo 50 aina ya Di-Ammonium Phosphate (DAP) nayo imepanda kutoka Sh3,000 hadi Sh3,200 huku kilo 25 za mbegu zikipanda hadi Sh4,750 kutoka Sh4,500.

You can share this post!

BI TAIFA FEBRUARI 22, 2021

Huenda maelfu wakafa njaa Tigray, UN yaonya