UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Vigezo muhimu katika kutathmini insha-2

Na ENOCK NYARIKI

KATIKA makala yaliyotangulia, tulianza kuangazia vigezo muhimu vinavyotumiwa katika utathmini wa insha za wanafunzi katika mtihani.

Tulieleza kwamba ni muhimu wanafunzi kuvifahamu vigezo hivi kama njia moja ya kuyajua matarajio ya watahini na kujiandaa vyema ili kuyakidhi matarajio hayo. Tuliangazia maudhui, mtindo na muundo katika muktadha wa insha.

Tulifafanua kwamba maudhui ni jumla ya mambo au hoja zinazojitokeza katika insha. Tuliona jinsi maudhui yalivyo kigezo muhimu katika insha ya mwanafunzi. Aidha tulitoa tofauti baina ya muundo na mtindo jinsi vipengele hivi viwili vinavyoeleweka katika muktadha wa insha. Muundo ni muonekano wa insha ilhali mtindo ni jinsi au namna ya kuandika insha. Mbinu mbalimbali za urutubishaji wa insha, jinsi ya kuiwakifisha kazi ya mwanafunzi, unadhifu miongoni mwa mambo mengine ni jumla ya mambo yanayozingatiwa wakati wa kuitathmini insha kwa kukitumia kigezo cha mtindo.

Katika makala haya, tutaangazia mtiririko na mshikamano jinsi dhana hizo zinavyoeleweka katika uandishi wa insha na zinavyotumiwa kama vigezo muhimu katika kuitathmini insha. Mtiririko ni mfuatano wa vitushi au mawazo katika insha. Insha nzuri ni ile inayomwongoza msomaji kutoka wazo moja hadi jingine. ‘Wazo’ ni kipengele kimoja kati ya vingi vinavyojitokeza katika insha. Insha ya masimulizi kwa mfano huwa na kisa kimoja kikuu ambacho kimejengwa kwa mawazo mbalimbali ambayo katika muktadha huu tutayaita maudhui. Jinsi kisa kinavyopangiliwa kutoka aya moja hadi nyingine hadi kufikia mwisho wa insha ndio unaoitwa mtiririko.

Katika insha ambazo zimejikita katika hoja, mtitiriko huangaliwa kutokana na namna hoja hizo zilivyopangana na kufuatana kutegemea uzito wazo kutoka aya moja hadi nyingine. Kila hoja sharti ishughulikiwe na kukamilishwa katika aya moja.

Kila wazo vivyo hivyo linapaswa kutajwa mara moja bila kurudiwarudiwa isivyo lazima. Uandishi mzuri ni ule wa kukisema kile unachotaka kukisema na kukisema mara moja. Mawazo katika insha ya mwanafunzi hayapaswi kuwa na ‘mruko wa panzi’(hakika hii ni tafsiri ya moja kwa moja ya ‘grasshopper-like-jumps’). Ni makosa kuitenga hoja moja katika aya kadhaa wakati ambapo ilihitajika kushughulikiwa katika aya moja tu.

Utengaji wa moja katika aya tofauti utaifanya insha kutokuwa na mtiririko unaofaa. Ili kuhakikisha kuwa insha ina mtiririko mwafaka, mwanafunzi anashauriwa kujizoeza kuyaandika chini mawazo wanayotaka kuayaelezea kwa njia ya vidokezi.

Vidokezi hufanya kazi ya dira inayomwongoza mwanafunzi kujua ni wazo gani linalofuata jingine na ni aya gani inayofuata nyingine. Insha yenye mtiririko mbaya ni kama chakula kisichokuwa na ladha. Anayekila chakula hicho hukila ahlan wasahalani tu bila kukifurahia. Kwa hivyo, ili insha iyanase mawazo ya mtahini, sharti mwandishi wa insha yenyewe amakinikie sana mtiririko.

Matumizi ya mbinu ya taharuki ni njia mojawapo ya kukifanya kisa kuvutia na kuwa na mtiririko mzuri. Mwanafunzi ajiepushe na uandishi unaonasibiana na ule wa mhazili au sekeretari anayemwandikia bosi wake kumbukumbu. Uandishi wa aina hii( ule wa sekeretari anayeandika kumbukumbu)humshurutisha mtu kuyajumuisha mambo yote yaliyojadiliwa hata yale ambayo si muhimu!

Mshikamano

Hakika, mtiririko na mshikamano ni vipengele viwili vinavyokurubiana sana. Mshikamano ni jinsi mawazo yanavyofuatana kutoka neno hadi neno, kutoka sentensi hadi nyingine na kutoka aya hadi aya. Kimsingi, mtiririko huzingatia jinsi mawazo hayo yanavyofuatana kutoka aya hadi nyingine hadi kufikia tamati ya insha ilhali mshikamano huiangalia insha kwa uwazi, kwa ukina na kwa upana zaidi. Mshikamano huangalia uelewano uliopo baina ya maneno, baina ya tungo na baina ya vifungu.

Kwa muhtasari, mtiririko mzuri ni mfano wa ramani au dira ambayo humwongoza mtu na kumfikisha hata mahali ambapo hajawahi kufika. Insha yenye mtiririko na mshikamano mbaya wa mawazo humchosha na kumchusha msahihishaji; jambo ambalo huishia kuathiri alama za mwanafunzi katika insha. Makala yajayo yatashughulikia kipengele cha sarufi na hijai pamoja na matumizi ya msamiati na misemo.

Habari zinazohusiana na hii