ONYANGO: Baraza la Kiswahili liundwe kupitia BBI

Na LEONARD ONYANGO

MNAMO Agosti 2018, Baraza la Mawaziri liliidhinisha kubuniwa kwa Baraza la Kitaifa la Kiswahili ambalo lilifaa kutwikwa jukumu la kukuza na kuendeleza lugha hiyo adhimu.

Baraza la Mawaziri lilieleza Wakenya kwamba lilipitisha pendekezo hilo kwa kuzingatia Kifungu cha 137 cha Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambao unahitaji lugha ya Kiswahili ikuzwe na kutumiwa na mataifa yote ya Jumuiya.

Miaka miwili baada ya kupitishwa kwa pendekezo hilo, baraza la Kiswahili limesalia ndoto – kwani baado halijabuniwa.

Rais Uhuru Kenyatta amesalia na chini ya miaka miwili afisini na huenda akastaafu Agosti, mwaka ujao, bila kuunda baraza hilo.

Ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) iliyozinduliwa Oktoba, mwaka jana, inasema kuwa kuna haja ya kuendeleza na kukuza lugha ya Kiswahili ili tuweze kujivunia kama Waafrika.

Ripoti hiyo inapendekeza kwamba serikali iweke mikakati ya kuhakikisha kuwa vitabu vilivyoandikwa kwa Kiswahili pamoja na lugha nyinginezo za kiasili, vinasomwa katika taasisi za elimu humu nchini.

Lugha ya Kiswahili imeunganisha Wakenya kwa kiwango kikubwa. Bila Kiswahili, ingekuwa vigumu kwa watu kutoka jamii mbalimbali humu nchini kutangamana.

Katiba ya 2010, ilikipa Kiswahili hadhi ya juu kwa kukifanya kuwa lugha ya taifa na lugha rasmi. Hiyo inamaanisha kuwa Wakenya wanaweza kutumia Kiswahili katika afisi yoyote nchini wanapotafuta huduma.

Lugha ya Kiswahili inazidi kukua na kuwanda kote barani Afrika. Mataifa mbalimbali, yakiwemo Namibia na Afrika Kusini, sasa yanafundisha lugha ya Kiswahili shuleni. Hiyo inamaanisha kuwa nafasi za ajira kwa walimu wa Kiswahili zinazidi kuongezeka.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa, wiki iliyopita, aliambia Bunge la nchi hiyo jirani kuwa serikali imeanza mikakati ya kufungua vituo vya kufundishia Kiswahili katika balozi zake kote duniani.

Serikali ya Kenya pia inafaa kuiga Tanzania kwa kufungua vituo vya mafunzo ya Kiswahili katika balozi zake. Hatua hiyo itatoa nafasi za ajira kwa maelfu ya Wakenya.

Lakini hilo halitawezekana bila kuwa na baraza letu la Kiswahili sawa na Baraza la Kiswahili la Tanzania (Bakita).

Janga la virusi vya corona lilipovamia nchi yetu mnamo Machi 2020, kwa mfano, wanahabari, wanafunzi na Wakenya walilazimika kutohoa maneno kama vile sanitaiza (vitakasa) na maski (barakoa) kabla ya kubaini majina ya Kiswahili. Kuna uwezekano kwamba majina hayo – vitakasa na barakoa – yalitokea Tanzania.

Mfumo mpya wa elimu ya 2-6-6-3 umekuja na madarasa mapya kama vile ‘Junior Secondary’ na ‘Senior Secondary’. Wasomi wa Kiswahili watavutana kwa muda kabla ya kuafikiana kuhusu majina mwafaka.

Mvutano huo ungeepukwa ikiwa tutakuwa na Baraza la Kiswahili la Kenya (Bakike) ambalo litatafiti msamiati ibuka wa Kiingereza na kupata maneno yake ya Kiswahili.

Habari zinazohusiana na hii